Wednesday, January 31, 2018

RC MASENZA ASHAURI MATUMIZI YA TEHAMA MAHAKAMA KUU IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ameishauri Mahakama kuu kanda ya Iringa kuongeza kasi ya matumizi ya Tehama katika utoaji wa haki kwa wananchi.

Kauli hiyo aliitoa katika salamu zake kwenye uzinduzi wa wiki ya sheria nchini uliofanyika katika uwanja wa Mahakama kuu Iringa jana.
 

Masenza alisema kuwa faida za Tehama katika Mahakama ni kurahisisha utoaji haki kwa wakati kwa wananchi. Aliongeza kuwa Tehama inasaidia kutunza kumbukumbu muhimu za mwenendo wa kesi na hatimae utolewaji wa haki. 

Tehama inaimarisha mawasiliano miongoni mwa wadau. Ni rahisi kuwapa taarifa wadau huko waliko wakahudhuria Mahakamani kwa wakati pale wanapohitajika bila taarifa kupotea. Tehama huimarisha maadili ya utoaji wa haki kwa wananchi, vifaa kama CCTV camera na vifaa vingine vya aina hiyo ni muhimu katika kuimarisha maadili ya haki” alisisitiza Masenza.

Katika hotuba ya Jaji mfawidhi wa Mahakama kuu kanda ya Iringa, mheshimiwa Mary Shangali alisema kuwa wiki ya sheria nchini imelenga Mahakama kujipambanua kwa wananchi na kueleza majukumu ya Mahakama na kutoa elimu kwa wananchi kuwa mahkama kuu ya Tanzania ipo kwa ajili ya wananchi na haki zao.

Mheshimiwa Shangali aliongeza kuwa wiki hiyo inalenga kupima utendaji kazi wa Mahakama. Alisema katika maadhimisho hayo, vituo vya kutolea elimu na kupokelea maoni ya wananchi vimeandaliwa katika shule ya sekondari ya wasichana Iringa, shule ya sekondari ya Miyomboni na chuo kikuu cha Iringa.
=30=    
  

No comments:

Post a Comment