Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Ofisi
ya mkuu wa Mkoa wa Iringa imepongezwa kwa usimamizi makini unaozingatia thamani
ya fedha katika ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo unaoendelea.
Pongezi
hizo zilitolewa na makamu mwenyekiti wa kamati ya Bunge ya utawala na serikali
za mitaa, Mwanne Mchemba alipokuwa akiongea na wataalam wa Mkoa wa Iringa na
Wilaya ya Kilolo katika kumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo baada ya
kamati yake kukagua ujenzi wa hospitali hiyo hivi karibuni.
Mchemba
alisema kuwa ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Iringa imefanya kazi nzuri kusimamia
ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo.
“Najua
mipango mizuri ya ujenzi wa hospitali hii mliiratibu vizuri tangu mwanzo ndiyo
sababu ujenzi unaenda vizuri. Kamati yangu imeridhishwa na hatua ya ujenzi kwa
kuzingatia thamani ya fedha” alisema Mchemba.
Alipongeza wazo hilo kuwa
linalenga kuboresha afya za wananchi wa Wilaya ya Kilolo na taifa kwa ujumla
kwa kuwapatia huduma bora za afya.
Mchemba
aliishauri ofisi ya Rais TAMISEMI kutoa kipaumbele katika ujenzi wa chumba cha
upasuaji na chumba cha kuhifadhia maiti. Alisema kuwa ujenzi wa majengo hayo
utasaidia kuiwezesha hospitali hiyo kuanza ikiwa na maeneo muhimu ya utoaji
huduma. Aidha, alielekeza hospitali hiyo kupatiwa gari la wagonjwa.
“Kutokana na jiografia ya Wilaya ya Kilolo ni
muhimu hospitali ya Wilaya kupewa gari la wagonjwa. Gari hilo ni muhumu sana
kwa sababu litasaidia kuokoa maisha ya wananchi watakaohitaji huduma ya haraka
na dharura hospitali hapo” alisema Mchemba.
Awali
katika taarifa ya ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Kilolo iliyosomwa na mganga
mkuu wa Wilaya, Dr. Mohamed Mang’una alisema kuwa mradi huo ulianza kwa gharama
ya shilingi 259,451,899 kugharamia ujenzi awamu ya kwanza na ya pili. Alisema
kuwa kupitia ruzuku ya maendeleo ya serikali za mitaa kwa mwaka 2011/2012
zilitolewa shilingi 145,744,500 na mwaka 2012/2013 zilitolewa shilingi
113,707,399 kujenga jengo la wagonjwa wa nje.
Hospitali
ya Wilaya ya Kilolo imelenga kuhudumia wakazi wanaokadiriwa kuwa 229,146
kutokana na sense ya watu na makazi ya mwaka 2012.
=30=
No comments:
Post a Comment