Thursday, February 8, 2018

Makamu wa Rais Kuanza Ziara ya Siku Tano Mkoani Iringa



Anaandika Atley Kuni- TAMISEMI

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anatarajia kuanza ziara ya Kikazi kwa muda wa Siku tano Mkoani Iringa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenda kwa vyombo vya  habari na Mkuu wa mkoa wa Iringa Mh. Amina Masenza, imesema ziara hiyo pamoja na mambo mengine vilevile, Makamu wa Rais atapata fursa yakuongea na kusalimiana na wananchi wa mkoa huo
 
Mkuu wa Mkoa Amina Masenza
Masenza amesema, Mapokezi ya Mheshimiwa Makamu wa Rais yatafanyika kwenye Kijiji cha Kising’a Wilaya ya Iringa majira ya saa 3.45 asubuhi.

Ndugu zangu mara baada ya mapokezi  Makamu wa Rais atafungua wodi ya Kissing’a lakini pia atakagua upanuzi wa kiwanda cha IVORY, sambamba na kukagua kiwanda cha ufungashaji mazao ya Mbogamboga na Jioni ya siku hiyo hiyo atapokea  taarifa ya Mkoa na kuzungumza na viongozi wa taasisi mbali mbali mkoani humo.

Mheshimiwa Masenza amefafanua kuwa katika siku yake ya pili Mheshimiwa  Makamu wa Rais ataelekea Wilaya ya kilolo ambapo atazindua jengo la utawala shule ya Sekondari kilolo na atafanya mkutano wa Hadhara katika eneo la Ilula.

Taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkuu wa Mkoa na kusambazwa katika vyombo vya habari imeonesha siku tarehe 11Februari 2018 Mhe. Makamu wa Rais ataweka jiwe la msingi katika maabara kwenye shule ya Sekondari Mgololo na atafungua zahanati ya Kijiji cha Mtili na kukagua kiwanda cha utengenezaji Mkaa Mafinga.

Masenza alifafanua kwamba katika siku zote hizo  Mheshimiwa Makamu wa Rais atapata pia fursa ya kuzindua mradi wa kuendeleza utalii ukanda wa kusini (REGROW) ambapo Mkoa wa Iringa ni kitovu cha Utalii utakaofanyika kwenye  eneo la kihesa kilolo kuanzia majira ya saa 3:00 asubuhi na majira ya saa  8:00 Mchana atafanya Mkutano wa Hadhara Mwembetogwa katika Manispaa ya Iringa.

Hata hivyo Mh. Masenza amefafanua kuwa, siku ya tarehe 13 Januari, 2018 atafanya majumuisho kabla yakuondoka mkoani humo.

Mh. Masenza amewaomba wananchi wa Iringa kujitokeza kwa wingi ili kumlaki kiongozi huyo wa Kitaifa.
“Natoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi na kwa shamrashamra, nderemo na vifijo na furaha tele wakati wa mapokezi na maeneo yote ya miradi anayotembelea ambapo atapata fursa ya kuwasalimia wananchi” amenukuliwa Masenza.

No comments:

Post a Comment