Thursday, March 26, 2015

MYUYU AWATAKA WATENDAJI WA KATA KUOMARISHA MAWASILIANO IRINGA



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Uimarishaji wa mawasiliano baina ya watendaji wa kata na maafisa tarafa umeelezwa kuwa ni nyenzo muhimu katika utekelezaji wa kazi za serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Menejimenti ya Serikali za Mitaa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bw. Wilfred Myuyu alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu majukumu ya watendaji wa kata katika usimamizi wa shughuli mbalimbali za maendeleo wilayani Kilolo.

Bw. Myuyu amesema kuwa katika kutekeleza majukumu, mtendaji wa kata anatakiwa kuwasiliana mara kwa mara na afisa tarafa. Amesema kuwa kwa mujibu wa miongozo ya mawasiliano serikalini, afisa tarafa anajukumu la kusimamia watendaji wa kata ili watekeleze majukumu yao ipasavyo. Amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya Tawala za Mikoa Na. 19 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2006 inaweka wazi kuwa majukumu ya afisa tafara ni kusimamia shughuli za watendaji wa kata, vijiji na mitaa katika eneo lake.

Akiongelea majukumu ya watendaji wa kata katika ujenzi wa maabara unaoendelea, Bw. Myuyu amesema kuwa watendaji wa kata wanawajibu wa kuwatambua wadau mbalimbali wa maendeleo wanaoweza kuchangia na kuwahamasisha kwenye shughuli za ujenzi wa maabara ikiwa ni pamoja na wananchi. Ameongeza kuwa wanalo jukumu la kufanya ufuatiliaji na tathmini ya ujenzi unaoendelea ili kujiridhisha na uzingatiwaji wa viwango kusudiwa pamoja na kasi ya ujenzi. Amesema kuwa katika ufuatiliaji huo wanalojukumu la kufahamu changamoto zilizopo kushauri na kuzipatia ufumbuzi.

Jukumu linguine amelitaja kuwa ni kuhakikisha michango inayotolewa na wananchi na wadau inatumika kwa kuzingatia taratibu zinazoongoza matumizi ya fedha za umma na kutoa taarifa ya matumizi ya fedha hizo kwa wananchi.    

Bw. Myuyu ameongeza kuwa jukumu lingine ni kutoa taarifa za maendeleo ya ujenzi wa maabara juu ya hatua za utekelezaji zilizofikiwa, changamoto zilizopo na hatua za utatuzi wa changamoto.
=30=

No comments:

Post a Comment