Monday, July 30, 2012

TAASISI ZA DINI ZATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO ILI KUFANIKISHA SENSA




Serikali Mkoani Iringa imeomba ushirikiano kutoka kwa viongozi wa dini katika kuhakikisha kuwa elimu ya kutosha na hamasa vinatolewa ili uelewa huo uwafikie waumini na wananchi wengi kwa ujumla.

Ombi hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiendesha zoezi la harambee ya ujenzi wa kanisa kuu la mtaa wa Wilolesi mjini hapa katika ibada ya kwanza iliyofanyika katika kanisa kuu, usharika wa Iringa Mjini.

Dkt. Christine amesema kuwa Tanzania itafanya Sensa ya Watu na Makazi tarehe 26 Agosti, mwaka huu na kuendelea kwa takriban siku saba. Amesema “Sensa ya Watu na Makazi ni utaratibu wa kukusanya, kuchambua na kusambaza takwimu za kidemografia, kiuchumi na kijamii kuhusiana na Watu wote na Makazi yao katika nchi kwa kipindi maalum”. Amesema kuwa Sensa hiyo ni zoezi lenye lengo la kupata idadi ya watu wote katika nchi, kwa umri na jinsi, mahali wanapoishi, hali yao ya elimu, hali ya ajira, hali ya vizazi na vifo na hali ya makazi. 

Akiongelea malengo ya Sensa hiyo, Mkuu wa Mkoa amesema “Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 inalenga kutathmini utekelezaji wa Mipango yetu mikubwa ya Maendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa katika kipindi kilichopita. Mipango hiyo ni pamoja na Mkakati wa Kupunguza Umasikini na Kukuza Uchumi Tanzania na Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar”.

Akiongelea nafasi ya kanisa katika kufanikisha Sensa hiyo, Dkt. Christine amesema “napenda kuongelea nafasi ya Kanisa katika kuhakikisha Sensa ya Watu na Makazi inafanikiwa. Ni kweli kuwa Kanisa linalo jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa zoezi hili linafanikiwa kwa sababu takwimu hizo ndizo zitakazoiwezesha Serikali kutambua hali halisi na mahitaji halisi ya huduma zilipo katika maeneo yenu hivyo kuingizwa katika Mipango ya Maendeleo ya Taifa”. Amesema “kwa msingi huo, ninawaomba sana kuwahamasisha waumini na wananchi kwa ujumla ili wahesabiwe na wahesabiwe mara moja tu, ili takwimu zitakazokusanywa ziwe sahihi”.

Ameyataja mambo muhimu ya kutiliwa mkazo wakati wa kuwahamasisha washarika na wananchi kwa jumla kuwa ni tarehe ya Sensa, umuhimu wa Sensa na yatakayojiri wakati wa zoezi la kuhesabu watu. Sensa hiyo ya Watu na makazi inaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Sensa kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa’.

No comments:

Post a Comment