Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, IRINGA
Mamlaka
ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi imetakiwa kuendelea kusimamia na kuratibu
mafunzo studi nchini ili mafunzo yanayotolewa yawe na ubora unaokidhi mahitaji
ya soko la ajira.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza katika hotuba yake
iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Tawala Msaidizi- Mipango na Uratibu katika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe katika mahafali ya 21 ya chuo
cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma Iringa yaliyofanyika katika viunga vya
chuo cha VETA mjini Iringa.
Mkuu
wa Mkoa alisema “kimsingi mamlaka ya
elimu na mafunzo ya ufundi stadi bado ina kazi kubwa ya kusimamia, kuratibu,
kugharamia, kutoa na kuendeleza mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kufikia dhamira
kuu ambayo ni kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakuwa na ubora unaokidhi
mahitaji ya soko la ajira”. Aidha, aliitaka mamlaka kuendelea kuboresha
fani nyingine zinazohitaji maboresha makubwa kama karakana ya magari.
Akiongelea
hitaji la wahitimu la kuunganishwa na fursa zinazohusu vijana ili kuwawezesha
kuendana na mbadiliko ya teknolojia na soko la ajira, alisema kuwa sualaa hilo
ni changamoto. “Suala hili ni changamoto
kwa mamlaka, wazazi na hata wahitimu pia. Ninapenda kutumia mahafali haya
kuwashauri wazazi kushiriki kikamilifu kuwasaidia ninyi katika hali ya mmoja
mmoja, lakini nikishauri zaidi kwamba ninyi wahitimu kuunda na kusajili vikundi
vyenye utaratibu mzuri wa usimamizi na uzalishaji wenye faida ambavyo vitaweza
kuwapa fursa ya kupata mitaji kupitia taasisi mbalimbali za kifedha pamoja na
mifuko ya vijana inayosimamiwa na halmashauri zetu” alisema mkuu wa Mkoa.
Akiongelea
ombi la serikali kugharamia mafunzo ya vitendo, mkuu wa Mkoa alisema kuwa suala
hilo linahitaji majadilianao na mamlaka husika. Aidha, aliwakumbusha wazazi
kuwa wanawajibu wa kuwasaidia watoto wao kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Katika
risala ya wahitimu wa chuo hicho iliyosomwa na Geofrey Simon ilieleza kuwa
changamoto ni kutokuwa na walimu wa kutosha kukidhi mahitaji na uwiano sahihi
katika kufundisha baadhi ya masomo. Alisema kuwa jambo hilo hupelekea walimu
waliopo kuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha idadi kuwa ya wanafunzi katika
masomo ya hisabati, kiingereza, ujasiriamali na michoro ya maumbo. Changamoto
nyingine ni chuo kukosa gari la kusafirishia wanafunzi waendapo kutembea maeneo
ya mafunzo na michezo.
Simon
aliongeza kuwa karakana nyingi za chuo zina vifaa na mitambo ya kufundishia
iliyopitwa na wakati na kufanya mafunzo kutokidhi ubora wa soko la ajira. “Serikali kutokuwadhamini wanachuo fedha ya
kufanya mafunzo ya vitendo, hivyo wazazi wengi kushindwa kumudu gharama husika
imekuwa ni changamoto kubwa” alisema Simon.
Katika
taarifa ya mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi na huduma iringa, Raphael
Ng’wandu alisema kuwa chuo chake kimefanikiwa katika kugharamia mafunzo kwa
wanafunzi wote waliodahiliwa. Alisema kuwa mamlaka imekuwa ikigharamia chakula
na malazi kwa wanafunzi wanaokaa bweni.
Ng’wandu
alisema kuwa chuo chake kinakabiliwa na changamoto ya kuwa na vifaa vya muda
mrefu visivyoendana na teknolojia ya sasa. Alisema kuwa chuo chake kina mkakati
wa kuboresha karakana za mafunzo kwa kununua vifaa vipya vya mafunzo vya
kufundishia. Aidha, mamlaka imeendelea kuboresha bajeti ya mafunzo mwaka hadi
mwaka.
Chuo
cha mafunzo ya ufundi stadi cha Iringa kilianzishwa mwaka 1987 chini ya idara
ya mafunzo na majaribio ya ufundi (NVTD) iliyokuwa chini ya wizara ya kazi.
Fani za kwanza kutolewa zilikuwa ni uashi, bomba, useremala na umeme.
=30=
No comments:
Post a Comment