Sunday, November 26, 2017

TANZANIA MSTARI WA MBELE KUPINGA UBAGUZI KWA WATOTO NA WANAWAKE



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa-IRINGA
Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuheshimu haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya watoto na wanawake.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika maelezo yake wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia uliyofanyika ngazi ya mkoa katika halmashauri ya Wilaya ya Kilolo na kusomwa na Afisa maendeleo ya jamii katika Ofisi ya mkuu wa mkoa, Saida Mgeni.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa nchi ya Tanzania ipo mstari wa mbele katika kuheshimu haki na utu wa mwanamke kwa kutekeleza mkataba wa umoja wa mataifa wa kupinga aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na watoto ambao Tanzania imeusaini na kuuridhia. 

Serikali kwa kushirikiana na wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika ya hiyari na watu binafsi wamekuwa wakitumia kampeni hii kuhamasisha jamii kwa lengo la kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto. Alisema kuwa maadhimisho haya yalenge kutafakari mafanikio na changamoto zinazoikabili jamii na kuandaa mkakati wa kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia Januari 2016-septemba, 2017, wanawake 904 wamefanyiwa ukatili wa aina moja au nyingine. Aliongeza kuwa ukatili wa kijinsia unachangia maongezeko ya maambukizi ya virusi vya ukimwi. 

Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye kiwngo kikubwa cha mambukizi ya vvu. Watu wenye umri wa miaka 15-49 ambao ni asilimia 9.1 na maambukizi ya wanawake ni asilimia 10.2 ikilinganishwa na asilimia 6.9 ya wanaume. Kitaifa ni asilimia 5.1 ambapo wanawake ni asilimia 6.3 na wanaume asilimia 3.5” alisisitiza Katibu Tawala Mkoa.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ilizinduliwa ngazi ya Mkoa, katika Kijiji cha Lyasa, Kata ya Image Wilaya ya Kilolo chini ya kaulimbiu ya isemayo ‘funguka! Ukatili dhidi ya wanawake na watoto haumuachi mtu salama chukua hatua’.     
=30=

No comments:

Post a Comment