Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Kamati
za uendeshaji wa mitihani ngazi za Wilaya na Mkoa zimepongezwa kwa usimamizi
madhubuti wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi na kudhibiti udanganyifu.
Pongezi
hizo zilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa wanafunzi wanaotarajia
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa
akifungua kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini
Iringa jana.
Ayubu
alisema kuwa mwaka 2017 Mkoa wa Iringa haukukumbwa na tuhuma za udanganyifu. “Kipekee nazipongeza kwa dhati kamati za
uendeshaji wa mitihani za Wilaya na ya Mkoa kwa usimamizi mzuri. Nitoe wito
kuwa usimamizi huu uendelee kwa mitihani
ya kitaifa ya ngazi zote ili kuepukana na suala la udanganyifu ambalo kwa kiasi
kikubwa madhara yake ni makubwa kwa mwanafunzi mwenyewe, mwalimu aliyehusika na
udanganyifu na Taifa kwa ujumla” alisema Ayubu.
Akiongelea
idadi ya wanafunzi waliofanya mtihani, alisema kuwa
watahiniwa
24,784 (wavulana 11,421 na wasichana 13,363) sawa na 99.5% walifanya mtihani.
Aliongeza watahiniwa 20,606 (wavulana 9513 na wasichana 11,093) sawa na
asilimia 83.14 wamefaulu mtihani huo. Alisema wanafunzi walioshindwa kufaulu mtihani
huo ni 4,178 ikiwa wavulana 1,908 na wasichana 2,270 sawa na asilimia 16.86
“Kiwango
cha ufaulu kimeongezeka kwa asilimia 0.27 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka
jana ambapo ufaulu ulikuwa ni 82.87%. Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza
wadau wote wa elimu katika Mkoa wetu ambao mchango wao ni mkubwa kwa ongezeko
hili la ufaulu na kuufanya Mkoa wetu kuwa wa Nne (4) kitaifa kati ya mikoa 26
ya Tanzania bara alisema Ayubu.
Mwaka
2017 Mkoa wa Iringa ulikuwa na watahiniwa 24,905 waliosajiliwa kufanya mtihani,
wakiwemo wavulana 11,490 na wasichana 13,415 katika shule 481.
=30=
No comments:
Post a Comment