Saturday, December 16, 2017

WADAU WA VVU/UKIMWI IRINGA WATAKIWA KUJITATHMINI



Na Ofisi ya mkuu wa Mkoa
Wadau wa mapambano dhidi ya maambukizi ya VVU na Ukimwi wametakiwa kujitathmini katika utekelezaji wa mkakati wa kupambana na VVU baada ya mbinu za awali kuonesha kushindwa.

Kauli hiyo ilitolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akifungua kikao cha kuutambulisha mradi wa USAID Tulonge Afya kilichofanyika katika hoteli ya Gentle Hills iliyopo mjini Iringa.
 
RAS Wamoja Ayubu
Ayubu alisema matokeo ya utafiti wa VVU na UKIMWI (2016/2017) yameonesha kuwa maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 hadi 11.3. “Maambukizi ya VVU mkoani Iringa yameongezeka kutoka asilimia 9.1 ya awali (2011/12) kufikia asilimia 11.3 (2016/17). Hii ni ishara wazi kuwa maambukizi mapya yameongezeka kwa asilimia 2.2” alisema Ayubu.

Aidha, aliwataka wadau wa mapambano dhidi ya VVU kujitathmini ili kuona maeneo ambayo hawakufanya vizuri. 

Tunatakiwa tujitathmini kuona ni wapi ambapo hatujafanya vizuri katika utekelezaji wa program zetu za mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU” alisema Ayubu.

Katibu Tawala Mkoa alisema kuwa wadau wa maendeleo wamekuwa wakitoa mchango mkubwa katika kuwaletea maendeleo na kuboresha afya za wananchi mkoani Iringa. 

Uwepo wenu katika Mkoa huu umeongeza kasi ya serikali ya Mkoa na Halmashauri zake ya kuwafikia wananchi katika jitihada zao mbalimbali za kukabiliana na changamoto za maisha, hasa kujikwamua kiuchumi na kuimarisha afya zao” alisema Ayubu.
=30=

No comments:

Post a Comment