Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Iringa
Mkoa
wa Iringa umefanikiwa kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watahiniwa wa mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017 kwa asilimia 0.27 na kushika nafasi ya nne
kitaifa.
Kauli
hiyo ilitolewa na mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa wanafunzi wanaotarajia
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2018 mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu katika
hotuba yake ya ufunguzi kwenye ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Ayubu
alisema “watahiniwa 20,606 (wavulana 9,513
na wasichana 11,093) sawa na asilimia 83.14 wamefaulu mtihani huo. Hali kadhalika
walioshindwa kufaulu mtihani huo ni 4,178 ikiwa wavulana 1,908 na wasichana 2,270
sawa na asilimia 16.86.
Kiwango hiki cha ufaulu kimeongezeka kwa
asilimia 0.27 ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana ambapo ufaulu ulikuwa ni
82.87% ninapenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza wadau wote wa elimu katika
Mkoa wetu ambao mchango wao ni mkubwa kwa ongezeko hili la ufaulu na kuufanya
Mkoa wetu kuwa wa Nne kitaifa kati ya mikoa 26 ya Tanzania bara”.
Ayubu
ambaye pia ni Katibu Tawala Mkoa wa Iringa alisema kuwa ongezeko hilo la ufaulu
ni jambo jema na kutahadharisha kuwa linaibua changamoto ya uhitaji mkubwa wa
vyumba vya madarasa katika shule za sekondari. “Ongezeko la ufaulu ni jambo jema kwetu lakini linaibua changamoto ya
uhitaji mkubwa wa vyumba vya madarasa katika shule zetu za sekondari au ujenzi
wa shule mpya za Sekondari ili kuweza kuwachukua wanafunzi wote waliofaulu
kujiunga na kidato cha kwanza” alisema Ayubu.
Aidha,
aliwataka wajumbe kuangalia jinsi ya kuongeza vyumba vya madarasa au kujenga shule
za sekondari maeneo ambayo yamekuwa na wanafunzi wengi wanaofaulu hasa mijini.
Aliongeza kuwa ongezeko la ujenzi wa vyumba vya madarasa liambatane na uongezaji
wa meza na viti ili kuhakikisha wanafunzi wote wanapata meza na viti.
Mkoa
wa Iringa ulikuwa na watahiniwa 24,905 waliosajiliwa kufanya mtihani wa
kumaliza elimu ya msingi mwaka 2017, kati yao wavulana 11,490 na wasichana
13,415 katika shule 481.
=30=
No comments:
Post a Comment