Saturday, November 17, 2012



MKOA WA IRINGA WAZIDI KUFANIKIWA KATIKA SEKTA YA KILIMO
Mkoa wa Iringa umeendelea kupata mafanikio makubwa katika Sekta ya Uchumi na Uzalishaji mali kwa kuongeza matumizi ya zana za kilimo hadi kufikia asilimia 15 kwa wakazi wa Mkoa huo.

 Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa Scolastica Mlawi akifafanua jambo.

Mafanikio hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa, Scolastica Mlawi wakati akifungua kikao cha siku mbili cha kupitia taarifa za uekelezaji wa kazi za Sehemu ya uchumi na sekta za uzalishaji na kuainisha vipaumbele kwa mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Scolastica amesema “mafanikio kwa upande wa sekta ya kilimo ni pamoja na ongezeko la matumizi ya zana za kilimo ambapo kwa sasa asilimia 15 ya wakazi wa mkoa huu wanatumia matrekta makubwa na madogo katika Kilimo”. Amesema asilimia 20 ya wakazi wanatumia wanyamakazi na asilimia 65 wanatumia jembe la mkono ikilinganishwa na asilimia 75 ya wakulima waliokuwa wanatumia jembe la mkono mwaka 2005.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa amesema kuwa pato la mkoa wa Iringa limeongezeka toka Sh. 867,482 mwaka 2005 hadi kufikia Sh. 1,985,708 mwaka 2011, wakati pato la mkazi mwaka 2005 lilikuwa Sh. 558,444 na limeongezeka hadi kufikia Sh. 1,125,503 mwaka 2011.
Akiongelea maandalizi ya kilimo msimu huu, amesema kuwa msimu wa kilimo umeanza na wakulima wameonesha jitihada kubwa katika kulima na kupanda mazao mbalimbali ya chakula na biashara.

Amesema “msimu huu tunajipanga zaidi katika kuhimiza mazao yanayostahimili ukame kama vile alizeti, mtama, muhogo na viazi vitamu. Kwa pamoja tuhimize kilimo cha mazao haya katika maeneo yote yenye ukame (upungufu wa mvua) katika wilaya zote hasa wilaya ya Iringa (Tarafa ya Idodi, Isimani na Pawaga), wilaya ya Kilolo (Tarafa ya Mahenge na Mazombe) wilaya ya Mufindi (Tarafa ya Sadani na Malangali)”.

Akiongelea ufanisi wa kilimo Scolastica amesema “ili kilimo chetu kiweze kufanikiwa vizuri tunahitaji kuwaelimisha wakulima wetu mbinu bora za kilimo ikiwemo matumizi bora na sahihi ya pembejeo za Kilimo”.

Awali Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Sekta ya Uchumi na Uzalishaji, Adam Swai alisema kuwa lengo la kikao hicho ni kutoa taarifa za utekelezaji wa kazi kutoka katika Halmashauri za wilaya ili kujadili tathamini, matokeo na kubadilishana uzoefu wa shughuli na kutoa ushauri wa pamoja katika  kuboresha utekelezaji wa shughuli na kupata takwimu halisia katika sekta ya uchumi. Aidha, amesema kuwa kikao hicho kitasaidia katika kuandaa taarifa ya Mkoa itakayoonyesha vipaumbele vichache ambavyo vitaleta matokeo na mafanikio.
=30=

No comments:

Post a Comment