Saturday, November 17, 2012

RC AKEMEA UKWEPAJI KODI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kuachana na tabia ya kukwepa kulipa kodi na kuwa wazalendo kwa mkoa wao na Taifa lao kwa ujumla wakati akikemea tabia ya wafanyabiashara wanaokwepa kutumia mashine za kieletroni za kutolea risiti.


Mkuu wa Mkoa amesema hayo katika hotuba yake kwenye maadhimisho ya siku ya mlipakodi iliyofanyika katika ukumbi wa chuo kikuu huria tawi la Iringa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dkt. Leticia Warioba.

Dkt. Warioba amesema “bado wapo walipakodi ambao sio wazalendo.Walipakodi ambao mpaka sasa wanakwepa kodi. Tabia hii ya kukwepa kodi siyo ya kizalendo na ningependa kuwaasa muiache mara moja”. Amesema kuwa ukadiliaji na ukusanyaji wa kodi vinafanyika kwa mujibu wa sheria za kodi na ni muhimu kwa kila mlipa kodi kuheshimu sheria na taratibu nchi ilizojiwekea.

Amesema tabia ya kukwepa kodi imekuwa ikiwafanya wafanyabiashara kupitisha bidhaa vichochoroni badala ya kupitisha bidhaa hizo kwenye ofisi za forodha zilizopo mipakani. Amesema kuwa utaratibu huo unafanyika kinyume na sheria za nchi na kutaka tabia hiyo iachwe mara moja.

Akiongelea matumizi ya mashine ya kieletroniki za kutolea risiti, Dkt. Leticia amesema “matumizi ya mashine hizo ni changamoto katika utendaji kazi wa Mamlaka ya Mapato nchini, ningependa kuwafahamisha kuwa, matumizi ya mashine hizi ni agizo la Serikali na lengo lake ni kuhakikisha kodi ya ongezeko la thamani inakusanywa ipasanyo”.

Amewataka wale wote waliosajiliwa na kodi ya ongezeko la thamani kutumia mashine za kieletroniki za kutolea risiti kwa kila mauzo wanayofanya. Amesema kuwa mashine hizo zinatumika kwa mujibu wa sheria ya bunge hivyo utekelezaji wake ni lazima.

Wakati huohuo, Mamlaka ya Mapato Mkoa wa Iringa imefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya zaidi ya asilimia 100 ya lengo iliyowekewa la idara ya ushuru wa forodha na kodi za ndani. Katika maelezo ya Meneja wa mamlaka ya mapata Mkoa wa Iringa, Rozalia Mwenda amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2011/2012 Mkoa wa Iringa ulipangiwa kukusanya jumla ya shilingi  23,761,800,000/= lengo la idara ya ushuru wa forodha likiwa shilingi 110,100,000/= na lengo la idara ya kodi za ndani likiwa shilingi 23,651,700,000/=. Amesema kwa kipindi hicho Mkoa ulikusanya shilingi 24,730,752,185 sawa na asilimia 105 ya utendaji.

Akiongelea ubora wa huduma kwa wateja, Rozalia amesema “mamlaka ya mapato makao makuu, mikoani hadi wilayani, inatekeleza sera ya ubora ambayo inaelekeza utendaji kazi wenye lengo la kutoa huduma bora inayokidhi na hata kupita matarajio ya mteja”. Amesema “baada ya kufanyika  kwa ukaguzi wa ubora wa huduma zetu na kampuni ya wakaguzi wa nje, mamlaka ilitunukiwa cheti cha kimataifa cha ubora wa viwango cha ISO 9001:2008”. Amesema kuwa mamlaka yake imepanga kutathmini mara kwa mara viwango vya huduma tunazotoa kwa walipa kodi ili kuhakikisha kuwa mahitaji ya walipakodi yanazingatiwa katika mipango ya mamlaka ya kimkakati.

Amesema kuwa mamlaka yake inaendeleza ushirikiano baina yake na mlipakodi kwa lengo la kudumisha ushirikiano wa kulipa kodi kwa mujibu wa sheria kwa kutoa huduma bora. Amesisitiza kuwa urafiki baina mamlaka na mlipakodi sharti uongeze tija katika kukusanya mapato ya Serikali kwa lengo la kutokumuumiza mlipa kodi na wala Serikali.

Meneja wa mamlaka ya mapato mkoa wa Iringa ameahidi kuongeza juhudi katika utendaji kazi, amesema “mimi na wafanyakazi  wa mamlaka ya mapato Mkoa wa Iringa tunaahidi kuongeza, juhudi, maarifa na uadilifu katika kuhakikisha tunavuka malengo tuliyopangiwa kama tulivyokwishaonesha kipindi kilichopita. Kwa mshikamano na mikakati tuliyonayo, tunaamini malengo ya mwaka 2012/2013 ambayo ni shilingi 33.4 bilioni yanafikiwa”.

Wiki ya maadhimisho ya 6 ya sherehe ya mlipakodi kitaifa ilianza tarehe 01-07 Novemba, 20122 ikiongozwa na kaulimbiu isemayo “ulipaji kodi wa hiari Kwa Taifa lenye mafanikio” ikiwa na lengo kuu la kuboresha huduma kwa mlipakodi.
=30=

No comments:

Post a Comment