Mikoa ya Iringa na Njombe imejipanga
kuhakikisha kuwa mitihani ya kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2012 inafanyika
katika hali nzuri na kutokuruhusu mianya yoyote ya udanganyifu na kusababisha
kufutiwa kwa matokeo kwa baina ya shule za msingi.
Akifafanua maandalizi ya mitihani
hiyo ofisini kwake, Afisa Elimu Mkoa wa Iringa, Mwalimu Joseph Mnyikambi
aliyepewa pia jukumu la kusimamia mitihani hiyo kwa mikoa ya Iringa na Njombe
amesema kuwa tayari semina zimeendeshwa na kamati ya usimamizi wa mitihani ya
mkoa katika Halmashauri zote nane za mikoa ya Iringa na Njombe. Amezitaja
Halmashauri hizo kuwa ni Njombe, Mufindi, Makete, Ludewa, Kilolo, Iringa, Njombe
Mji na Iringa Manispaa.
Akiongelea
maandalizi amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika na leo ndiyo siku ya
kuwapeleka wasimamizi katika vituo vyao ya kusimamia mitihani hiyo. Amesema
“kwa mujibu wa sheria zetu huwezi kumwambia msimamizi atasimamia wapi mtihani
huo”. Amesema kuwa lengo ni kuzuia udanganyifu na hongo kutoka kwa jamii kwenda
kwa msimamizi na kutoka kwa msimamizi kwenda kwa jamii pamoja na wanafunzi.
Kuhusu
taratibu, Mwalimu Mnyikambi amesema kuwa taratibu ni za kawaida na zilizozoeleka
isipokuwa kitu kipya ni mwaka huu watahiniwa wote watatumia penseli na fomu
maalumu kujibu mitihani hiyo kwa kusiliba kwa sababu kwa mara ya kwanza
itatumika teknolojia mpya ya ‘optical mark reader’ (OMR). Amesema kuwa majibu
yatasahihishwa kwa kutumia kompyuta.
Amesema
kuwa mitihani hiyo itafanyika kwa siku mbili na itaanza kesho tarehe 19 -20
Septemb, 2012. masomo yatakayotahiniwa ameyataja kuwa ni Sayansi, Hisabati na
Kiswahili. Mengine ni Kiingereza na Maarifa ya Jamii.
Ni kwa namna gani mkoa umejipanga kukabiliana
na udanganyifu unaoweza kusababisha wanafunzi kufutiwa matokea, Afisa elimu
mkoa wa Iringa amesema “kama mkoa tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa
udanganyifu haufanyiki katika mikoa ya Iringa na Njombe kwa kuzingatia taratibu
zote za mitihani”. Ameitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kila
mwanafunzi kukaa katika dawati lake na kukaa mmoja ili kuondoa uwezekano wa
kutizamiana. Amesema katika semina kwa wasimamizi wa mitihani, msisitizo
ulikuwa ni kuhakikisha hakuna udanganyifu wowote utakaopewa nafasi katika
mtihani huo ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayeingia kidato cha kwanza anajua
kusoma na kuandika na anakwenda kwa kufaulu vizuri.
Mwalimu Mnyikambi ameitaja idadi ya wanafunzi
watakaofanya mitihani hiyo ya kumaliza elimu ya msingi kwa mikoa ya Iringa na
Njombe kuwa ni 43,499 kati yao wasichana ni 23,015 na wavulana ni 20,484.
amesema jumla ya shule zote ni 887.
=30=
No comments:
Post a Comment