Wilaya ya Kilolo imeshauriwa kulima mazao yanayovumilia ukame ili kukabiliana na ukame unaoendelea kuinyemelea wilaya hiyo.
Ushauri huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma wakati akiongea na wafanyakazi wa Serikali kuu na Halmashauri Wilayani Kilolo alipofanya ziara ya kujitambulisha na kuzifahamu changamoto zinazoikabili Wilaya hiyo.
Dkt. Ishengoma amesema “lazima tutafute mazao yanayostahimili ukame, lazima twende katika kilimo cha mtama”. Amesema “lazima tumfikirie mwananchi wa Kilolo atapataje chakula cha kutosha, bahati mbaya huwa sipendi sana tabia ya kuomba omba chakula cha msaada sababu si staha kwa mtu mzima”.
Aidha, ameishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kuangalia uwezekano wa kununua mbegu bora za mtama na kuweka utaratibu mzuri ambao watautumia kwa wakulima ili uweze kuwanufaisha. Amesema kwa mujibu wa vituo vya utafiti mbegu bora ya mtama si nyingi sana kwa sababu sehemu nyingi za nchi zimekumbwa na ukame na kusababisha maeneo mengi kulazimika kununua mbegu ya mtama.
Ameushauri uongozi wa Wilaya ya Kilolo kuwashawishi wananchi kununua mbegu bora za mtama na kuzipanda kwa vitendo.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema “tumepata njaa kwa sababu hatutumii kilimo cha umwagiliaji”. Amesisitiza matumizi mazuri ya skimu za umwagiliaji ili kujihakikishia chakula cha kutosha. Kilimo cha umwagiliaji kinamuwezesha mkulima kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka na kujihakikishia uhakika wa chakula.
Akiongelea usindikaji wa mazao amesema kuwa usindikaji huo unaongeza thamani ya mazao husika.
Amewataka maafisa Mipango kushirikiana na kuandika maandiko ya miradi midogo midogo ili kuweza kuyaongezea mazao thamani. Amesema “ni lazima tuweke mikakati ya kuwainua wananchi, si lazima mpaka wananchi waibue wenyewe sisi wataalamu tunaweza kuwajibika kwa niaba ya wananchi”.
No comments:
Post a Comment