Askofu mteule wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kusini Njombe ameazimia kuanzisha ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda wa kusini ili kuendeleza na juhudi za kanisa katika kuiletea jamii ustawi.
Kauli hiyo imetolewa na Askofu mteule Isaya Japhet Mengele baada ya kusimikwa kazini na Mkuu wa KKKT nchini Askofu. Dk. Alex Malasusa katika kanisa kuu, Dayosisi ya Kusini-Njombe.
Akiongelea mipango yake ya baadae Askofu Mengele amesema ni ujenzi wa chuo kikuu cha dayosisi katika ukanda huo wa kusini ili kuwanufaisha wananchi wengi katika sekta ya elimu.
Aidha, akiongelea dhana ya kilimo kwanza, Askofu. Mengele ameipongeza serikali kwa hatua hiyo na kuishauri kuwa kilimo kwanza ili kitoe matokeo mazuri kifanyike kwa kanda kutokana na mazao yanayozalishwa katika kanda husika ili kuongeza chachu na kuinua kilimo ili kiwanufaishe wananchi wengi zaidi.
Akiongelea sekta ya elimu amesema ataendelea kushirikiana na serikali katika kuboresha utoaji wa elimu nchini. Aidha, ameishauri Serikali huongeza kasi katika kuifanya hospitali teule ya Ilembula kuwa hospitali ya rufaa ikiwa ni pamoja na kuisaidia gari la kubebea wagonjwa ili kuwasaidia wananchi wengi.
Katika salamu za Mkoa wa Iringa, zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma, amempongeza Askofu mteule Mengele kwa uteuzi wake. Aidha, amewaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla wao kukaa chini na kutafakari juu ya nchi na kuiombea ili iendelee kuwa na amani, upendo na utulivu.
Vilevile, Dk. Ishengoma imelishukuru kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania kwa michango na ushiriki wake katika kuiletea maendeleo jamii. Ameitaja michango hiyo kuwa ni pamoja na kuijenga jamii katika maadili na kuwafanya wananchi wake kuwa raia wema, mingine ni elimu na afya.
Nae Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Mkuchika aliyemuwakilisha Waziri Mkuu aliyepo safarini nchini Brazili amewataka viongozi wa dini kukemea maovu, na kuwataka waumini kufuata mfundisho ya dini na kujitolea kulijenga kanisa lao na nchi yao .
No comments:
Post a Comment