HOTUBA YA MGENI RASMI KATIBU TAWALA MKOA WA IRINGA GERTRUDE K. MPAKA WAKATI
WA KUFUNGA MAFUNZO YA SENSA YA WATU NA MAKAZI MWAKA 2012 KWA WAANDISHI WA
HABARI WA KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI PAMOJA NA MIKOA YA LINDI NA MTWARA
YALIYOFANYIKA CHUO KIKUU RUAHA IRINGA,
TAREHE 13 AGOSTI, 2012
Ndugu Mwenyekiti,
Mratibu wa Mratibu wa
Sensa Mkoa,
Watendaji kutoka
Ofisi ya Taifa ya Takwimu,
Watendaji kutoka
Sekretarieti ya Mkoa,
Ndugu Washiriki wa
Mafunzo,
Mabibi na Mabwana,
Ndugu Mwenyekiti,kwanza
kabisa sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana hapa na kuhudhuria
mafunzo haya hadi kufikia hatua ya mwisho yaani hatua ya kumaliza. Aidha nachukua fursa hii kuwashukuru sana washiriki
wote kwa kuheshimu mwaliko wa kuhudhuria mafunzo haya muhimu ambayo yalihusu
maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 na nafasi ya vyombo vya
habari katika kufanikisha zoezi hilo.
Ndugu Mwenyekiti,
nilipopata mwaliko kuwa Mgeni Rasmi kufunga mafunzo haya kwanza nilifurahi kwa
kuwa niliona nimepata fursa ya pekee kukutana na kundi kubwa la waandishi wa
habari kwa pamoja kitu ambacho ni nadra kutokea katika kutekeleza majukumu
yangu ya kila siku. Pili nimefarijika na mwaliko wenu kwa kuwa utanipa fursa ya
kuchangia mawazo katika baadhi ya maeneo ambayo yamezungumziwa katika mafunzo
haya.
Ndugu Mwenyekiti, mafunzo
haya nimeelezwa kuwa yamezungumzia maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi
iliyopangwa kufanyika tarehe 26 Agosti, 2012. Nimeelezwa kuwa jumla ya mada
tano ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina ambapo pia washiriki walipata fursa
ya kufanya mazoezi kwa vitendo kwa baadhi ya mada walizojifunza.
Kwa ujumla nimeelezwa kuwa mada
zote ziliibua majadiliano na hoja mbali mbali pamoja na changamoto za hapa na
pale lakini jambo muhimu ni kuwa lengo la majadiliano hayo yalilenga katika
kujifunza zaidi na kuongeza ufahamu kwa kila mshiriki juu ya masuala ya msingi
kuhusu Sensa. Mimi naamini kuwa wataalamu wetu hapa kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu wamejitahidi kadri ya utaalamu wao na uwezo waliojaaliwa na Mwenyezi
Mungu kuyafafanua kinagaubaga masuala yote yanayohusu Sensa ambayo yalihitaji
maelezo ya ziada ya yale yaliyowasilishwa. Mbali ya maelezo ya wataalamu
nimeelezwa kuwa mmepatiwa nyaraka muhimu zenye kueleza na kufafanua masuala ya
msingi ya Sensa. Nyaraka hizo zitawasaidia kuongeza ufahamu wenu kuhusu suala
zima la Sensa.
Ndugu Mwenyekiti, kwa
mantiki hiyo ninaamini kuwa ndugu washiriki mmefaidika na maelezo hayo na sasa mmekamilika
katika suala zima linalohusu maandalizi ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka
2012. Maana yake ni kuwa sio tu mko katika nafasi nzuri ya kuandika na kutangaza
kwa usahihi habari za Sensa lakini pia mafunzo haya yatakuwa yamewatia shime na
ari ya kushiriki katika kufanikisha Sensa ya Watu na Makazi mwaka 2012.
Matarajio yetu basi ni kuona taarifa zaidi za Sensa hasa zile za kuhamasisha
wananchi kushiriki zinatolewa mara kwa mara katika vyombo vya habari nchini na
hususan vyombo vyetu vilivyomo katika mikoa ya kanda yetu.
Ndugu Mwenyekiti,
nafasi niliyopewa ni kuyafunga mafunzo haya lakini kabla ya kufanya hivyo
ningependa kusisitiza mambo mawili. Jambo la kwanza ni suala la ushirikiano. Waswahili tuna msemo usemao ‘kidole kimoja
hakivunji chawa’. Kama ilivyoelezwa na wataalamu, mafanikio ya Sensa
yanategemea sana ushiriki na ushirikishwaji wa kila mdau katika nchi. Kwa maana
hiyo ni ukweli usiopingika kuwa Serikali pekee haiwezi kufanikisha Sensa kwa
sababu mchakato wake ni mkubwa unaohitaji ushiriki wa wadau wa kila aina na
kutoka sekta mbalimbali. Miongoni mwa wadau hao ni vyombo vya habari.
Hivi sasa nchi yetu inajivunia
utajiri mkubwa wa vyombo vya habari ambavyo ni matokeo ya mabadiliko ya sheria
ya umiliki wa vyombo habari iliyopitishwa na Serikali. Dhamira ya Serikali
kufanya marekebisho hayo ni kuwapa fursa zaidi watanzania kushiriki katika
ujenzi wa taifa kwa kuamini kuwa vyombo hivi vitatumika kuwaendeleza wananchi
kwa kuwaelimisha, kuwahabarisha na kuwaburudisha.
Historia ya nchi yetu inaonyesha
kuwa vyombo vya habari vimekuwa mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada za
Serikali sio tu katika kuboresha hali ya maisha ya kila mwananchi bali pia
katika kuimarisha uzalendo na mshikamano miongoni mwa wananchi. Hivyo, wito wa
Serikali kwa vyombo vya habari ni kuviomba viendeleze ushirikiano na mshikamano
wa watanzania kama vinavyovyofanya katika masuala mengine yenye maslahi na
Taifa letu ili kufanikisha Sensa.
Ndugu Mwenyekiti,
naelewa kuwa Serikali haina shaka hata kidogo kuhusu uwezo wa vyombo vya habari
katika kulieleza jambo hili kwa usahihi kwani mnalifahamu na kwa mafunzo na
uzoefu mlionao nyinyi ni walimu na wasemaji wazuri hivyo tumieni ujuzi na uwezo
wenu huo kuwaeleza wananchi kwa ufasaha kuwa Sensa ni muhimu kwao na kwa Taifa
lao hivyo wasisite kushiriki. Kwa hiyo, matarajio ya Serikali ni kuona kuwa
mnakuwa waelimishaji wazuri na wahamasishaji makini wa Sensa ili kila mwananchi
kwa hiari yake aone kuwa ana wajibu wa kuhakikisha anahesabiwa na anahesabiwa
mara moja tu.
Ndugu Mweneykiti,
Jambo la pili ni suala la kutoa taarifa sahihi na kwa wakati. Leo zimebaki siku 12 tu kufika siku ya Sensa tarehe
26 Agosti 2012. Hivyo vyombo vya habari na wasemaji wote wa Sensa hawana budi
kuepuka kufanya makosa katika uhamasishaji na zaidi walenge katika mambo muhimu
ambayo mwananchi anapaswa kuyafahamu. Mambo hayo aliyaeleza Mkuu wa Mkoa wakati
alipofungua mafunzo haya nami sina budi kuyarudia ili kuweka msisitizo.
1.0
Kuwa Sensa ya Watu
na Makazi itafanyika tarehe 26 Agosti, 2012.
2.0
Watakaohesabiwa ni
wale tu watakaokuwa nchini usiku wa Jumamosi tarehe 25 Agosti kuamkia Jumapili
tarehe 26 Agosti, 2012.
3.0
Watakaohesabiwa
katika Kaya ni wale watakaokuwa wamelala katika Kaya usiku wa kuamkia Siku ya
Sensa ambao, kama nilivyoeleza awali, ni usiku wa Jumamosi ya tarehe 25 Agosti,
2012 kuamkia Jumapili terehe 26 Agosti, 2012 pamoja na wanakaya wanaofanya kazi
za usiku ambao kwa usiku ule hawakulala kwenye Kaya. Hawa ni pamoja na watumishi wa sekta ya afya,
ulinzi na usalama na hata sekta ya habari.
4.0
Ni muhimu Mkuu wa
Kaya akaweka kumbukumbu sahihi za watu wake wote zikiwemo za umri,kiwango cha
elimu, ajira anayofanya, mahali anaposhinda mwanakaya wakati wa mchana na kwa
wanawake hali zao za uzazi.
Ndugu Mwenyekiti, mwisho, ningependa kueleza furaha yangu kwa washiriki wote kwa kuonyesha
ushirikiano mkubwa na uvumilivu wakati wote wa mafunzo. Ushirikiano na
uvumilivu wenu huo ulikuwa muhimu katika kufanikisha mafunzo haya hadi sasa
tunayafunga rasmi. Nichukue fursa hii kuwatakia safari njema wageni wetu wote
kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini na wenzetu kutoka mikoa ya Lindi na
Mtwara.
Baada ya kusema hayo naomba sasa
nitamke kuwa Mafunzo ya Sensa ya Watu na Makazi kwa waandishi wa habari wa
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini pamoja mikoa ya Lindi na Mtwara yamefungwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza
SENSA KWA MAENDELEO:
JIANDAE KUHESABIWA
No comments:
Post a Comment