Wahasibu
nchini wametakiwa kubadilika na kuendana na mabadiliko ya kimfumo hasa
imapoanzishwa kwa ajili ya kuboresha ufanisi wa kazi na kupunguza upotevu wa
fedha za Serikali.
Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa alipokuwa akiongea na
maafisa wa Serikali Mkoani Iringa muda mfupi kabla ya kuhudhuria Mahafari ya Chuo
kikuu cha Ruaha Iringa (RUCO).
Akifafanua
kuhusu changamoto za mfumo wa Epicor 9.05 katika utekelezaji wa kazi za
kihasibu na malipo, Dkt. Mgimwa ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kalenga amesema
kuwa lengo la Serikali kuanzisha mfumo huo ni kuhakikisha ufanisi katika
matumizi ya fedha za serikali na kuondoa mianya ya upotevu wa fedha hizo. Amesema
“tumekuwa na kipindi kifupi sana cha kuwawezesha wahasibu wetu juu ya kuutumia
mfumo wa Epicor 9.05”. Akiufafanua mfumo huo, amesema kuwa mfumo huo ulianzia
Marekani mwaka 1996 na kuanzishwa nchini kutokana na uwezoz wake wa kuchukua
maagizo ya kimalipo kwa wingi, ukubwa, wepesi na haraka na sifa yake nyingine
ni kukidhi viwango vya kihasibu vya kimataifa. Amesema kuwa mfumo huo pia
unauwezo mkubwa wa kuhifadhi taarifa nyingi kwa wakati.
Amesema kuwa ili kuweza
kuenda vizuri na mfumo huo ni lazima wahasibu wakubali kubadilika na kuwa
wepesi zaidi kuyakubali mabadiliko hayo.
Akiongelea
uidhinishwaji wa fedha za miradi ya maendeleo ambao umekuwa ukilaumiwa sana
kuwa umekuwa ukichelewa sana, Waziri wa Fedha amesema kuwa mchanganuo wa
matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo ni muhimu sana na ndio unaozingatiwa
kabla ya kuidhinishwa malipo wengine ya miradi ya maendeleo. Amesema kuwa
thamani ya fedha ni jambo linalopewa uzito katika miradi yote ya maendeleo ili
fedha ya serikali inayotolewa iendane na mradi uliokusudiwa. Amesema kuwa
changamoto iliyopo katika kodi ya Serikali ikihusishwa na miradi ya maendeleo,
amesema “tunaruhusiwa kutoa asilimia tano tu iliyopatikana na kupeleka katika
miradi ya maendeleo na asilimia nyingine inabaki kwa ajili ya kulipa mishahara
na shughuli nyingine za uendeshaji wa Serikali” amesisitiza Dkt. Mgimwa.
Kaimu
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Nuhu Mwasumilwe ameelezea changamoto inayoukabili
Mkoa wa Iringa kuwa ni ukomo wa bajeti hasa katika miradi ya maendeleo. Amesema
kuwa katika miradi ya maendeleo fedha hizo zimepungua kutoka shilingi bilioni 1
hadi milioni 274. Ametolea mfano miradi inayoendelea kuwa ndiyo inayoathirika
zaidi, kama ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa mwaka 2012/2013
imetengewa shilingi milioni 51 tu kati ya milioni 700 zinazohitajika.
Aidha,
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Iringa ameiomba Hazina kuwa inatoa kipaumbele kwa
miradi ya maendeleo inayoendelea. Akiongelea fedha za matumizi ya kawaida
amesema kuwa kupungua kwa fedha hizo kumekuwa kukisababisha kutokueleweka
katika maeneo mengine ikiwa ni pamoja na Ofisi za Wakuu wa Wilaya. Amesema
mfano mwaka 2011/ 2012 fedha za matumizi mengine Mkoa ulipangiwa shilingi
bilioni 2.7 ingawa hazikutolewa zote. Aidha, mwaka 2012/2013 Mkoa umepangiwa
shilingi bilioni 1.9.
Nae
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amempongeza Waziri wa Fedha
kwa kuteuliwa kwake katika nafasi hiyo na kuomba ushirikiano wa viongozi na
wadau wote katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
=30=
No comments:
Post a Comment