Thursday, September 21, 2017

WADAU WAOMBWA MICHANGO KUFANIKISHA UTALII NA KAZI ZA VIWANDA VIDOGO



Na. Dennis Gondwe, IRINGA
Wadau wa maendeleo ya utalii mikoa ya nyanda za juu kusini wameombwa kuchangia maonesho ya Utalii Karibu Kunisi na shughuli za wajasiliamali wa viwanda ili yafanikiwe na kuchangia katika uchumi wa Taifa.

Ombi hilo lilitolewa na katibu msaidizi wa kamati ya maonesho ya utalii mkoa wa Iringa, Hawa Mwechaga alipokuwa akikabidhi stakabadhi ya malipo kwa mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Jackson Ngowi katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa jana.

Mwechaga alisema “nichukue nafasi hii kwa niaba ya Katibu Tawala mkoa wa Iringa, kumshukuru Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo kwa mchango wake wa shilingi milioni moja fedha taslimu katika kufanikisha maonesho ya Utalii Karibu Kusini na shughuli za wajasiliamali wa SIDO”. Alisema kuwa wadau wa utalii na biashara wana nafasi nzuri kuchangia katika kufanikisha maonesho hayo kwa sababu watafahamika na kukuza biashara na huduma wanazofanya.

Mwechaga alisema kuwa kupitia sekta ya utalii inayokuwa kwa kasi nchini, wadau wameweza kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa na kuwafikia wananchi wengi zaidi. Lakini kupitia maonesho ya utalii wananchi wengi wameweza kupata maono mapya ya kufanya kazi za kiutalii na wengine kuboresha kazi walizokuwa wakifanya awali.

Maonesho ya Utalii Karibu Kusini mwaka 2017 yatafanyika mkoani Iringa kwa pamoja na maonesho ya shughuli za wajasiliamali wa viwanda vidogo (SIDO) yakihusisha mikoa ya nyanda za juu kusini katika uwanja wa Kichangani mjini Iringa kuanzia tarehe 27/9/2017 -02/10/2017.
=30=  

No comments:

Post a Comment