Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
Iringa
Serikali
imeandaa mkakati wa kuendeleza biashara ndogo kwa lengo la kufikia uchumi
unaotegemea viwanda ifikapo mwaka 2025.
Kauli
hiyo ilitolewa na mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza alipokuwa akifungua
maonesho ya wajasiriamali wadogo na wa kati katika uwanja wa mashujaa mjini Mafinga
jana.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza akikagua bidhaa katika Maonesho ya wajasiriamali mjini Mafinga |
Masenza
alisema kuwa katika nchini nyingi duniani, asilimia kubwa ya pato la watu binafsi
linatokana na biashara ndogo na za kati.
“Hivyo kuendeleza
sekta hii ni mkakati wa kutimiza malengo
ya dira ya maendeleo ya kuwa na uchumi imara unaotegemea uzalishaji katika viwanda ifikapo 2025” alisema Masenza. Aidha, aliwataka SIDO
kuandaa mkakati wa kuwasaidia wajasiriamali waweze kupata masoko ya kudumu
ndani na nje ya nchi.
Akiongelea changamoto ya uingizaji bidhaa
kutoka nje, mkuu wa mkoa alisema kuwa uzalishaji wa bidhaa nyingi ndiyo
suluhisho la kujitegemea kwa mkoa wa Iringa. Alisema kuwa uzalishaji huo
utapunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi na kuongeza matumizi ya malighafi
zinazozalishwa ndani kutumika katika viwanda vya ndani.
“Utaratibu huu utasaidia kulinda viwanda vyetu wenyewe bila kutegemea
masoko ya nje tu kwa baadhi ya malighafi zetu” alisema mkuu wa mkoa.
“Katika
kipindi hiki chenye changamoto za kiuchumi duniani tujitahidi kuzalisha bidhaa
kwa wingi na zenye ubora wa hali ya juu ili kuongeza ajira na pato la Taifa.
Wananchi wote, wafanyabiashara na viongozi mliobahatika kutembelea maonesho
haya, hii ni fursa nzuri ya kuweka miadi na kununua au kuchangia mawazo yenu
katika kuboresha bidhaa zetu za hapa nchini, ili kusaidia kujenge msingi imara
wa viwanda na uchumi wetu” alisisitiza mkuu wa mkoa.
Maonesho ya wajasiriamali kwa mkoa wa Iringa
ni ya kwanza ya aina yake yaliyoandaliwa na T-LED, SIDO, TCCIA, TWCC kwa kushirikiana na Halmashauri ya mji wa Mafinga.
=30=
No comments:
Post a Comment