Friday, January 1, 2016

TADB YATOA MIKOPO YA KILIMO IRINGA




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa - IRINGA
Sekta ya kilimo ni muhimili wa uchumi nchini pamoja na kukabiliwa na changamoto nyingi katika ukuaji wake hasa upatikanaji mikopo.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakati wa utiaji saini makubaliano ya mikopo kati ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania na wakulima wadogo wadogo wa mkoa wa Iringa katika kijiji cha Igomaa wilayani Mufindi.
 
Mkuu wa Mkoa wa Irirnga, Amina Masenza
Masenza alisema “ikumbukwe kuwa umuhimu wa sekta ya kilimo unachagizwa na ukweli kuwa ni sekta ambayo inaajiri zaidi ya asilimia 75 ya wananchi wanaoishi vijijini, ambao wanategemea kilimo, ufugaji na uvuvi kwa ajili ya maisha yao. Kadhalika, wakulima, wafugaji na wavuvi wanatumia zana na mbinu duni katika shughuli zao, hivyo kushindwa kupata matokeo mazuri ya mazao”. Aliongeza kuwa pamoja na mchango mkubwa wa wakulima kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, kwa mujibu wa takwimu zilizopo kuhusu hali za maisha ya wakulima nchini siyo ya kuvutia hata kidogo. Wengi mapato yao yapo chini na wanaishi maisha duni sana.

Lengo la serikali ya awamu ya tano ni kuimarisha sekta ya kilimo ili iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika uchumi wa nchi na kuwanufaisha wakulima, wafugaji na wavuvi katika kuyabadilisha maisha yao  kwa kupitia mikopo na pembejeo za kisasa na mbegu bora zaidi. “Naamini ujio wa benki ya maendeleo ya kilimo (TADB) ni mwanzo tu wa maandalizi ya matokeo halisi ya ndoto na matamanio ya rais wetu, hivyo sina budi kuwapongeza na kuwaunga mkono katika hatua zote mnazozifanya katika kuwakopesha wakulima wadogo wadogo” alisisitiza Mkuu wa Mkoa wa Iringa.

Akiongelea changamoto iliyopo katika upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kilimo katika taasisi za kifedha, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, alisema kuwa upatikanaji wa fedha ni mgumu kutokana na mikopo mingi kuelekezwa katika biashara za bidhaa na riba kubwa kwenye mikopo ya kilimo. Aliongeza kuwa masharti ya dhamana ni kikwazo kikubwa kwa wakulima wadogo wengi. Alisema kuwa kuanzishwa kwa Benki ya Maendeleo ya Kilimo ni fursa kubwa kwa wakulima nchini.
=30= 

Monday, December 21, 2015

RC IRINGA AWATAKIA HERI MAJERUHI WA AJALI YA BASI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza amewatakia heri na kupona haraka majeruhi wote wa ajali ya basi ili waweze kuungana na familia zao na kuendelea na majukumu yao.

Kauli hiyo aliitoa muda mfupi baada ya kufanya ziara ya kustukiza katika hospitali ya rufaa ya Iringa kujionea jinsi majeruhi wa ajali ya basi la kampuni ya New Force wanavyohudumiwa hospitalini hapo.

Masenza akiyeambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa wa Iringa alisema kuwa ajali hiyo imemuhuzunisha yeye binafsi na mkoa kwa ujumla. Alisema kuwa anawaombea kwa Mungu majeruhi wote kupata nafuu na kupona kabisa ili waweze kuendelea na majukumu yao ya ujenzi wa Taifa.

Akiongelea hali ya huduma hospitali hapo, Masenza alisema kuwa ameridhishwa na jinsi majeruhi wa ajali hiyo walivyopokelewa na kutibiwa hospitalini hapo. Aidha, aliwataka madaktari na wauguzi kuendelea kuonesha moyo wa huruma na uwajibikaji wanapowahudumia majeruhi wa ajali hiyo. Aidha, aliwahakikishia majeruhi hao kuwa serikali ipo pamoja nao kuhakikisha wanapata huduma bora ili wapone haraka na kuendelea na majukumu yao.

Ajali hiyo ilitokea kwa basi kugongana na lori ilitokea tarehe 18 Disemba, 2015 mchana baada ya tairi la lori lori namba T 616 DES la kampuni ya Ranfad Ltd kupasuka kupasuka na lori kukosa muelekeo na kuligonga basi la kampuni ya New Force namba T 483 CTF na kusababisha vifo vya abiria 12 na majeruhi 28. Miongoni mwa majeruhi hao, watatu ni raia wa Kongo DRC na mmoja raia wa Afrika Kusini.

=30=

Wednesday, December 9, 2015

SIKU YA UHURU WA TANZANIA BARA ILIVYOADHIMISHWA MKOANI IRINGA

Wananchi wakifanya usafi katika kijiji cha Ruaha Mbuyuni A

Mkuu wa Mkoa wa Irirnga, Mhe. Amina Masenza akiwaongoza maafisa waandamizi kuelekea eneo la kufanya usafi

Zoezi la usafi likiendelea

Zoezi la usafi likiendelea

Mkuu wa Mkoa akichoma taka

Upande wa pili Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Bibi Wamoja Ayubu wanne (kulia) akiongoza vikosi vya usalama kuelekea eneo la kusanya usafi

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu wakwanza mbele (kulia)

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi (katikati) katika zoezi la usafi

Zoezini

Wananchi baada ya kuhitimisha zoezi la usafi

Baada ya zoezi la usafi

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Amina Masenza

Wananchi wakisikiliza nasaha za Mkuu wa Mkoa

Mkuu wa Mkoa akiongea na wananchi

Wadau wa sekta ya usafi wakifuatilia nasaha za Mkuu wa Mkoa

Mdau wa siku ya Uhuru wa Tanzania bibi Scolastica

Wananchi wakifuatilia nasaha za Mkuu wa Mkoa

Wananchi wakisikiliza nasaha za Mkuu wa Mkoa wa Iringa

Mkurugenzi Mtendaji (W) Kilolo, Rukia Muwango akijibu hoja za wananchi

Shaban Lubathillah Afisa Ushirika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa akifanya usafi katika Uso wa ofisi hiyo

Wednesday, November 18, 2015



TANGAZO

NDUGU WANA IRINGA

CHAMA CHA MADAKTARI WANAWAKE TANZANIA, WAKISHIRIKIANA NA WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII, WATAFANYA ZOEZI LA UPIMAJI WA HIARI WA SARATANI YA MLANGO WA KIZAZI KWA WAKINA MAMA WOTE WA MJINI IRINGA

ZOEZI HILI LITAFANYIKA KATIKA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA IRINGA NA HOSPITALI YA FRELIMO SIKU YA TAREHE 19-20/11/2015 KUANZIA SAA NNE ASUBUHI

ZOEZI HILI NI BURE

UKISOMA TANGAZO HILI MFAHAMISHE NA MWENZAKO.

ASANTE NA KARIBU SANA

Tuesday, November 17, 2015

TAARIFA KWA MGENI RASMI MHE. AMINA JUMA MASENZA MKUU WA MKOA IRINGA KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA CHOO DUNIANI, SIKU YA UNAWAJI MIKONO DUNIANI NA WIKI YA USAFI WA MAZINGIRA TANZANIA TAREHE 14/11/2015



Katibu Tawala Mkoa,
Mkuu wa wilaya
Katibu Tawala Wilaya
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Kilolo
Viongozi mbalimbali
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.

Mhe. Mgeni Rasmi; Uboreshaji wa huduma za Maji, Afya na Usafi wa Mazingira unajumuisha uboreshaji wa huduma zote za upatikanaji wa Maji safi na salama,  Matumizi ya vyoo bora, unawaji wa mikono kwa sabuni katika nyakati muhimu, Uboreshaji wa usafi wa Mazingira katika ngazi ya jamii na Taasisi.  Uboreshaji wa huduma hizi ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa kwa sababu huchangia kujenga afya bora kwa wananchi hivyo kuongeza nguvu kazi ya Taifa.
Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Robert Salim


Mhe. Mgeni Rasmi; katika kuhakikisha nchi yetu inafikia lengo la Milenia namba saba (7) ambalo linalenga kupunguza kwa nusu idadi ya watu ambao hawana huduma ya vyoo bora ifikapo mwaka 2015. Tanzania ilianzisha Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira ambayo ilizinduliwa na Mhe. Rais wa Awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete  tarehe 5 Juni 2012 yenye kauli mbiu ya Usafi ni Ustaarabu unaanza na sisi.  Kampeni hii inalenga kuongeza ujenzi wa vyoo bora katika kaya 1,520,000 na shule 812 ifikapo mwaka 2015.  Ambapo mkoa wa Iringa ulipewa lengo la kufikia kaya 41,984 Na shule 16
Mkoa wa Iringa ulianza kutekeleza kampeni hii mwaka 2012 kwa Halmashauri 2 za Wilaya ya Iringa na Mufindi zilianza utekelezaji.  Katika mwaka 2013 Halmashauri ya Manispaa ya Iringa na Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo zilianza utekelezaji na kufanya Halmashauri zote za Mkoa kuwa zinatekeleza Kampeni hii.  Kwa sasa jumla ya kata 33 kati ya kata 103 kutoka katika Halmashauri za mkoa wa Iringa zimeanza kutekeleza Kampeni hii. Hadi kufikia Septemba 2015 ni jumla ya kaya 21,727 (52%) ya lengo ziliboresha  vyoo vyake kupitia uhamasishaji shirikishi wa jamii “Uchefuaji.

Utekelezaji kwa kila Halmashauri ni Iringa MC kaya  3914 (48%), Iringa DC kaya 5,792 (44.8%), Mufindi kaya  9,613 (68%) na Kilolo kaya 2408 (34.5%).  Vilevile, jumla ya shule 52 zimeweza kujenga vyoo bora kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya mapato ikiwemo fedha maalum ya mfuko wa Kampeni ya Kitaifa ya Usafi wa Mazingira na jumla ya mafundi 191 wamepatiwa mafunzo ya ujenzi wa vyoo bora kwa kutumia Teknolojia rahisi. Aidha, Takwimu za hali halisi ya uwepo wa vyoo zinaonyesha kuwa jumla ya kaya 201,120 (89%) mkoani Iringa zinavyoo na kati ya hizo ni asilimia 17 tu ndiyo zenye vyoo bora.

Mhe. Mgeni Rasmi; Ukitaza taarifa  ya utekelezaji Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo ndiyo ipo chini katika utekelezaji.  Hivyo tumeamua kufanya maadhimisho haya katika wilaya hii ili kutoa hamasa kwa jamii iweze kujenga vyoo bora na kuboresha usafi wa mazingira kwa ujumla.  Aidha takwimu zinaonyesha kwamba katika kata ya Uhambingeto kaya 1227 (57%) kati ya kaya 2116 zina vyoo bora.  Na katika vijiji vyote vya kata hii hakuna kitongoji kilichoweza kufikia kuwa na kaya zote zenye vyoo bora ambalo ndiyo lengo kuu la Kampeni hii. Hali hii inahitaji jitihada za makusudi za uongozi wa kata na vijiji kuboresha hali ya usafi wa mazingira ili kujikinga na magnjwa yakuambukiza.

Mhe. Mgeni Rasmi; Maadhimisho ya Siku ya Choo Duniani, siku ya Unawaji Mikono kwa Sabuni Duniani na Wiki ya Usafi Tanzania ni moja ya  jitihada za Serikali katika kuhakikisha inafanya uhamasishaji wa jamii ili kuiwezesha kuchukua hatua ya kuzifanyia kazi changamoto zilizopo katika kuboresha huduma za maji, afya na usafi wa mazingira.

Kimatiafa siku ya kunawa mikono huadhimishwa kila tarehe 15 Oktoba na siku ya Choo Duniani huadhimishwa kila tarehe 19 Novemba.  Tanzania kwa kuzingatia umuhimu wa uboreshaji wa huduma hizi, iliamua kutenga wiki inayoanzia tarehe 13 hadi 19 Novemba kuwa ni wiki ya usafi Tanzania ambapo maadhimisho yake yalianza rasmi mwaka 2013.  Katika maadhimisho haya Tanzania huadhimisha kwa pamoja Siku ya Choo duniani, Siku ya kunawa Mikono Duniani na Wiki ya usafi Tanzania.

Mhe. Mgeni Rasmi;  Kauli mbiu ya maadhimisho haya huenda sambamba na kauli mbiu ya maadhimisho  ya Siku ya Choo Duniani  ambapo kwa mwaka  huu  kimataifa inasema “ USAFI WA MAZINGIRA NA LISHE. (SANITATION &NUTRITION) Kutokana na Mlipuko wa kipindupindu unaoendelea nchini, kauli mbiu ya Kitaifa imejikita katika ujumbe wa kutokomeza ugonjwa huo. Kauli mbiu hiyo ni “ KIPINDUPINDU HAKIKUBALIKI, PUNGUZA MAAMBUKIZI MAPYA, ZINGATIA USAFI WA MAZINGIRA.
Mhe. Mgeni Rasmi;  Katika kuadhimisha wiki hii shughuli mbalimbali za uhamasishaji zitakuwa zikifanyika shughuli hizo ni pamoja na:
·        Uhamasishaji wa nyumba kwa nyumba na utoaji wa elimu
·        Usafishaji wa pamoja na maeneo ya kuishi na taasisi
·        Usafishaji wa pamoja na maeneo ya wazi
·        Uelimishaji wa jamii kupitia matangazo ya redio
·        Usambazaji wa ujumbe kupitia vipeperushi na mabango unaohamasisha matumizi ya choo bora, usafi wa mazingira na kunawa mikono kwa sabuni nyakati tano muhimu.  Nyakai hizo ni kabla ya kutayarisha  chakula, kabla ya kula, kabla ya kumlisha mtoto, baada ya kutoka chooni na baada ya kumsafisha mtoto aliyejisaidia
·        Maonesho ya bidhaa mbalimbali za usafi wa mazingira.
·        Vilevile Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imeandaa warsha maalum kwa waandishi wa habari toka vyombo mbalimbali vya habari vya mkoa wa Iringa kwa lengo la  kufikisha ujumbe wa usafi wa mazingira kwa jamii katika wiki hii.
Aidha katika siku ya leo ya uzinduzi kutakuwa na Zoezi la unawaji wa mikono kwa kuhusisha watu wengi kwa lengo la kutoa Elimu na kuihamasisha jami juu ya njia sahihi ya unawaji mikono kwa sabuni.

Mhe. Mgeni Rasmi;
Naomba kuwasilisha.


Dkt. Robert Salim
MGANGA MKUU WA MKOA WA IRINGA.