Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa uchaguzi wa Mkoa wa Iringa, Barnabas Ndunguru Ofisini kwake leo. Ndunguru amefafanua kuwa wagombea nafasi za udiwani 13 kati ya 30 wa chama cha mapinduzi wamepita bila kupingwa katika Majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini. Wagombea 10 kati ya 12 wa CCM wamepita bila kupingwa katika jimbo la Kilolo na wagombea udiwani 11 kati ya 15 wamepita bila kupingwa katika Kata za jimbo la Njombe Kusini.
Mratibu huyo wa uchaguzi wa Mkoa wa Iringa ameongeza kuwa katika Majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini, Kata 17 zinawagombea zaidi ya mmojana hivyo zitafanya uchaguzi. Amevitaja vyama vitakavyoshiriki uchaguzi huo na idadi ya wagombea wake kuwa ni CCM (17), CHADEMA (9), NCCR- Mageuzi (5), TLP (3) na CUF (2). Aidha katika jimbo la Kilolo vyama vyenye wagombea ni CCM, CHADEMA, CHAUSTA, wakati katika jimbo la Njombe Kusini ni CCM, TLP na CHADEMA.
Wakati huohuo katika jimbo la Njombe Kusini aliyekuwa Naibu wa Spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mbunge wa jimbo hilo, Anne Semamba Makinda amefanikiwa kutetea nafahi hiyo baada ya kupita bila kupingwa. Nao Mgimwa Mahmoud Hassan (CCM) jimbo la Mufindi Kaskazini, na Kigola Mendrad Lutengano (CCM) jimbo la Mufindi Kusini wamepita bila kupingwa baada ya kushinda pingamizi zao dhidi ya wagombea ubunge Laurence Chumila (NCCR- Mageuzi) na Sanga Christian Aloyce wa majimbo ya Mufindi Kaskazini na Mufindi Kusini. Katika jimbo la Kilolo wanaowania jimbo hilo ni Profesa. Peter Mahamudu Msolla (CCM), Clay Meshack Mwitula (CHADEMA) na Mwaka Lameck Mgimwa (CHAUSTA).
Madiwani 13 wa CCM wapita bila kupingwa Njombe Kaskazini na Njombe Magharibi
Jumla ya wagombea nafasi za udiwani 13 wa chama cha mapinduzi wamepita bila kupingwa katika Kata zao ndani ya majimbo ya uchaguzi ya Njombe Kaskazini na Njombe Magharibi.
Taarifa hiyo imetolewa na Mratibu wa uchaguzi Mkoa wa Iringa, Barnabas Ndunguru ofisini kwake leo. Ndunguru amesema katika Jimbo la Uchaguzi la Njombe Kaskazini wagombea nadasi za udiwani 6 wa chama cha mapinduzi wamepita bila kupingwa na kuwataja majina yao kuwa ni Peter Luka Nyahuya (Kichiwa), Camilo Albino Hongoli (Mfriga), Chabiko Eliah Kyenga (Idamba), Richard Julius Chagavahye (Mahongole), Paulo Luhalagata Kinyamagoha (Ninga), Lunyamadzo Cheleso Mhidze (Ikondo) kati ya Kata 19 za Jimbo hilo. Katika Jimbo la Uchaguzi la Njombe Magharibi amewataja wagombea udiwani waliopita bila kupingwa kuwa ni Anna Upendo Edward Gombela (Mdundu), Frank Jeremia Lulandala (Wangama), Andrew Girson Mangula (SAJA), Elly Safari Chengula (Igosi), Enock Fungameza Kiswaga (Imalinyi), Abraham Lutangilo Chaula (Makoga), Lukengelo John Mgaya (Kipengere) kati ya Kata 17 za jimbo hilo.
Aidha Mratibu wa uchaguzi Mkoa wa Iringa amesema ushindani mkubwa upo katika vyama vya CCM, CHADEMA na CUF ambavyo vimesimamisha wagonbea katika majimbo mengi. Mratibu huyo ameongeza kuwa chama cha TLP kimesimamisha mgombea 1 katika Kata ya Lupembe na chama cha NCCR-Mageuzi kimesimamisha mgombea 1 katika Kata ya Luguda.
Kwa upande wa wagombea ubunge waliochukua fomu na kuteuliwa kugombea ubunge, Ndunguru amesema kuwa katika Jimbo la Njombe Kaskazini ni Deo Kasenyenda Sanga (CCM), Alatanga Ludaliko Nyagawa (CHADEMA), Hongole Ayubu, Godrey (CUF). Jimbo la Njombe Magharibi amewataja kuwa ni Gerson Hosea Lwenge (CCM), Thomas Simon Nyimbo (CHADEMA), Mhanga Jacob Lichano (CUF).
Mkoa wa Iringa una jumla ya majimbo 11 ya uchaguzi.
‘...Ndunguru awataka kufanya kazi kama familia moja!’
Watumishi wa Sehemu ya Utawala na menejimenti ya Rasilimali watu katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kuishi kama familia moja ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea katika ufanisi wa kazi.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu, Barnabas Ndunguru katika kikao cha Sehemu ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu kilichofanyika leo katika ofisi yake.
Ndunguru amesema “lazima tuishi kama familia moja sababu sisi ni kitu kimoja”. Ameongeza kuwa “muda tunaotumia kufanya kazi pamoja ni mwingi kuliko muda tunaotumia sehemu nyingine yoyote ikiwa ni pamoja na nyumbani hivyo sisi ni familia moja”.
Katibu Tawala huyo Msaidizi amesisitiza ushirikiano kwa watumishi katika utendaji kazi ili kufanikisha malengo aliyojiwekea kila mtumishi na malengo jumla ya ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Iringa. Aidha amesisitiza pia watumishi kufanya kazi kwa kufuata mpango kazi wa kila mtumishi ili kuondokana na dhana ya kulaumiana na kukinzana katika majukumu ya kila siku. Ameongeza kuwa kufanya kazi kwa kufuata mpango kazi wa kila mtumishi utachochea uwajibikaji unaolenga kutoa matokeo na Upimaji wa Wazi wa Utendaji Kazi wa Watumishi (OPRAS).
Watumishi wote wa Sehemu ya Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu wamekamilisha mpango wa mwaka na mpango kazi kwa kila mtumishi na kuukabidhi kwa Katibu Tawala Mkoa.
Timu ya RAS katika mazoezi mepesi
Timu ya michezo mbalimbali ya Katibu Tawala Mkoa wa Iringa maarufu kama (RAS Iringa) itakayoshiriki mashindano ya Shirikisho la Michezo kwa Wizara, Mikoa, Idara na Wakala mbalimbali wa Serikali (SHIMIWI) imeanza mazoezi mepesi ya kujiwinda ma michezo hiyo.
Afisa Michezo na Utamaduni wa Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa, Kenneth Komba amesema kuwa mazoezi hayo yalianza rasmi 4 Agosti, 2010 katika viwanja vya chuo kikuu kishiriki cha Elimu- Mkwawa kila siku ya juma kuanzia saa 9:30 alasiri hadi 11:30 jioni.
Komba ameitaja timu hiyo kuwa inajiwinda na michezo kama mpira wa miguu kwa wanaume chini ya kocha John Ndumbalo ambaye pia Katibu wa chama cha makocha mkoa wa Iringa, mpira wa pete kwa wanawake chini ya kocha Warda Sapali na kuvuta kamba wanawake na wanaume chini ya kocha Magret Msigwa.
Afisa Michezo na Utamaduni amesema kuwa mchujo wa awali kwa wachezaji utafanyika tarehe 13 Septemba na kusisitiza kuwa mchujo huo utazingatia mahudhurio katika mazoezi, uwezo wa mchezaji binafsi na nidhamu kwa mchezaji binafsi na timu.
Kwa upande wa mahudhurio amesema kuwa ni ya kuridhisha japokuwa watumishi wengi wanakabiliwa na majukumu mengi ya kikazi.
Mwandishi wa habari hiili amefanikiwa kufika katika viwanja vya chuo kikuu kishiriki cha elimu- Mkwawa na kuwakuta wachezaji wamehudhuria kwa kiwango cha kuridhisha na wakifanya mazoezi mepesi mepesi.
Komba amemuomba Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Rasilimali watu, Barnabas Ndunguru kuhudhuria na kushiriki katika mazoezi hayo ili kuleta hamasa kwa wanamichezo hao. Kwa upande wake Ndunguru amekubali ombi hilo na kuahidi kuwatembelea mara kwa mara.
Michezo ya SHIMIWI inatarajiwa kutimua vumbi tarehe 17 Septemba hadi Oktoba 2, 2010 jijini Tanga.
Good start man, keep it up!
ReplyDeleteKidumu Chama Cha Mapinduzi...umekuja huku kwetu pia??KARIBU SANA..
ReplyDelete