Friday, September 3, 2010

Mama Mpaka asisitiza elimu kwa wapiga kura pasina itikadi za kisiasa

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amekitaka chuo kikuu cha Tumaini Iringa kutoa elimu ya manufaa kwa wapiga kura pasipo kuingiza itikadi zinazolenga upande fulani wa chama chochote cha siasa.


Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Mama Gertrude Mpaka

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua warsha ya siku moja ya elimu ya mpiga kura kwa wilaya ya Iringa iliyofanyika katika ukumbi wa chuo cha ushirika tawi la Iringa.

Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, mama Gertrude Mpaka amesema “nawakata mtoe elimu ya manufaa kwa wapiga kura bila kuingiza itikadi zinazoelekea upande fulani wa chana chochote”. Ameongeza kwa kuwataka wafundishe mambo yote kwa mujibu wa mada zilizopitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na si vinginevyo.

Mama Mpaka amesisitiza kuwa elimu kwa wapiga kura ni muhimu sana kwa wananchi wote hasa waishio vijijini kwa sababu wananchi wengu wa vijijini hudanganywa wasichiriki katika uchaguzi. Aidha ameongeza kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi wengi kutokushawishiwa kuuza shahada zao za kupigia kura wala kushawishiwa kushiriki kuleta fujo wakati wa kampeni au uchaguzi na kufanya hivyo ni kinyume na sheria.

Katibu Tawala huyo wa mkoa wa Iringa amewataka wananchi wa Mkoa wa Iringa kutunza kadi zao za kupiga kura kama mboni ya jicho. Amesema “kadi hii inakupa utu, inakupa haki ya kumchagua kiongozi, unayemtaka na unayeona anafaa kuwa kiongozi”. Aidha amechukua nafasi hiyo kuwataka wananchi wa Iringa ifikapo tarehe 31 Oktoba, 2010 kwenda kupiga kura.

Amewataka waandaaji wa warsha hiyo kuwaeleza wananchi kuwa kila raia anayo haki ya kuchagua, kuchaguliwa na kusikilizwa anapotoa maoni yake kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Aidha amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika kampeni kusikiliza sera za wagombea ili kuwa na uelewa mpana wa sera na ilani za wagombea wate wa nafasi za uongozi.

Mama Mpaka amewakumbusha watumishi wa umma kuzingatia Waraka waMkuu wa Utumishi wa Umma Na. 1 wa mwaka 2000 unaohusu maadili ya watumishi wa umma katika mfumo wa vyama vingi vya siasa kuwa unawataka watumishi wa umma kutojihusisha na siasa mahali pa kazi.

Amewataka washiriki wa warsha hiyo kuzingatia mafundisho watakayoyapa na kwenda kuwafundisha wengine kwa usahihi mkubwa bila upotoshaji wa makusudi. Amekumbusha kuwa serikali imekemea vitendo vyovyote vya rushwa wakati wa uchaguzi na kuwataka wawe wasimamiaji wa sera na sheria za taifa zenye kudhibiti vitendo hivyo.

Warsha hiyo imeandaliwa na chuo kikuu cha Tumaini- Iringa baada ya kushinda tenda ya shirika la maendeleo la umoja wa mataifa (UNDP) inayosimamiwa na shirika la DELOITTE. Warsha hiyo inawahusisha maafisa watendaji wa kata za Kalenga, Nzihi, Ulanda, Mseke, Nduli, Nyang’oro na Kihorogota. Wengine ni walimu wa masomo ya uraia na waandishi wa habari kwa uwiano wa kijinsia.


Washiriki wa warsha ya elimu ya mpiga kura wilaya ya Iringa akisikiliza kwa umakini hotuba ya mgeni rasmi mama Gertrude Mpaka katika ukumbi wa chuo cha ushirika Iringa.

No comments:

Post a Comment