Thursday, October 21, 2010



Na Concilia Niyibitanga

Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo ambayo ndio yenye dhamana ya kusimamia vyombo vya habari nchini imeviasa kuepuka kuandika habari za uchochezi zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Hayo yamesemwa leo na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Sethi Kamuhanda wakati wa mahojiano maalumu yaliyolenga kujua mwenendo wa vyombo vya habari hususani katika kipindi hiki cha kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu.

Bw. Kamuhanda amesema kuwa moja ya kazi kuu za vyombo vya habari ni kuelimisha wananchi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu jamii yao na si kuandika habari zinazoweza kusababisha uvunjifu wa amani.

Amesema kuwa uhuru wa vyombo vya habari una mipaka yake kwani vyombo vya habari vinatakiwa kufuata sheria na kanuni za nchi husika ili kulinda amani na utulivu wa nchi husika.

Aidha, amesema kuwa Serikali haitavumilia chombo chochote cha habari kitakachojihusisha na kuandika habari kwa nia yakusababisha uchochezi kwani wananchi ambao ndio wasomaji na wasikilizaji wa vyombo hivyo wanaamini kuwa kila kinachozungumzwa na kuandikwa kwenye vyombo vya habari ni sahihi.

Bw. Kamuhanda amesema kuwa Serikali inatoa rai kwa vyombo vya habari vinavyoandika habari za uchochezi kujirekebisha ili amani iliyojengwa na viongozi wetu na wananchi kwa ujumla iendelee kudumu.

Hata hivyo, amevipongeza vyombo vya habari vinavyoendelea kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na kuwaelimisha wananchi masuala mbalimbali yanayohusu uchaguzi mkuu 2010.
 
© Michuzi | Wednesday, October 20, 2010 |

No comments:

Post a Comment