Wadau watakiwa kuliunga mkono jeshi la polisi Iringa
Serikali mkoani Iringa imewaomba wafanya biashara na wadau mbalimbali wa masuala ya amani kuliunga mkono jeshi la polisi na serikali katika jitihada za kupambana na uhalifu.
Ombi hilo limetolewa na Katibui Tawala Mkoa wa Iringa, mama Gertrude Mpaka aliyekuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa filamu ya msalaba wa maisha iliyoandaliwa na kikundi cha sanaa cha MUNDU kupitia polisi jamii/ ulinzi shirikishi uliofanyika katika ukumbi wa Highland manispaa ya Iringa.
Mama Mpaka amesema “napenda kuwaomba wafanyabiashara wote wa mkoa wa Iringa, wajitokeze kuunga mkono jeshi la polisi na serikali kwa ujumla katika mapambano na uhalifu wa aina yoyote”. Amesema jeshi la polisi baada ya kutoa elimu kupitia kitengo cha polisi jamii kwa njia ya redia, vipeperushi na mikutano, pia limeona ni vema kuwashirikisha vijana ili wapate ajira kupitia maigizo na filamu.
Katibu Tawala Mkoa ameyataja madhumuni ya filamu hiyo kuwa ni pamoja na kutoa elimu kwa wananchi hasa wakazi wa mkoa wa Iringa kutambua na kuachana na imani potofu zinazosababisha mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, watoto wachanga na vikongwe. Aidha ametoa rai kwa makundi yote yanayojihusisha na tabia hizo potofu na chafu na zinazokinzana na maadili ya jamii kuacha mara moja.
Amevitaka vyama vinavyotoa tiba asilia kufanya kazi zao kwa umakini pasi nakuingiza imani potofu na zinazojenga hofu katika jamii. Pamoja na mkoa wa Iringa kuwa na vyama viwili yaani chama cha waganga/wakunga wa tiba asilia Tanzania (CHAWATIATA) na chama cha waganga na wakunga wa jadi Iringa (C.W.W.I) tatizo lipo pale nani atakuwa tayari kuwajibika pale yanapotokea mauaji. “serikali inawashauri kufanya kazi zao chini ya mwamvuli mmoja, ili serikali iweze kuwabana waganga wanaopiga ramli chonganishi na kuchukua hatua stahili”.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 toleo la 2005 suala la haki ya kuishi, ulinzi na usalama yamesisitizwa: Ibara:14. haki ya kuwa hai, “kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake kwa mujibu wa sheria”. Ibara: 15. (1) kila mtu anayo haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru”.
Mama Mpaka amesisitiza kila mwana Iringa na jamii kwa ujumla kuifuata Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndiyo sheria mama na kutokomeza aina zote za uhalifu katika jamii. Amesisitiza kuwa jukumu la kuwalinda walemavu wa ngozi, watoto wachanga na vikongwe ni la jamii nzima na si la kuliachia jeshi la polisi pekee.
RAS akibonyeza kitufe kuzingua filamu ya Msalaba wa Maisha
No comments:
Post a Comment