Monday, March 7, 2011

Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimetakiwa kutoa kipaumbele katika shughuli za uboreshaji wa usafi wa mazingira kwa kuongeza ajira na bajeti isiyo chini ya asilimia 30 ya bajeti ya afya.

Kauli hiyo imetolewa na Afisa Afya wa Sekretarieti ya Mkoa wa Iringa, Theophil Likangaga wakati akiwasilisha mada juu ya Tuzo mashindano ya Afya na usafi wa Mazingira katika Kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika katika ukumbi wa SIasa ni Kilimo uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Katika kufikia mafanikio endelevu ya usafi wa wa mazingira katika Mkoa wa Iringa ni vizuri kwa “uongozi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kutoa kipaumbele katika shughuli za uboreshaji wa usafi wa mazingira kwa kuongeza ajira na bajeti angalau isiwe chini ya asilimia 30 ya bajeti yote ya idara ya Afya” alisisitiza Likangaga.

Aidha, alizisisitiza Halmashauri kuifanyia marekebisho mipango mikakati yao ya udhibiti wa taka ngumu na taka maji. Akiongelea changamoto zilizopo katika Afya na Usafi wa Mazingira, Afisa Afya huyo alizitaja kuwa ni pamoja na upungufu wa watumishi hasa maafisa Afya akitolea takwimu kuwa Katika Halmashauri za Mkoa wa Iringa zinaupungufu unaofikia asilimia 50 ya mahitaji. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni bajeti ndogo inayotengwa kwa shughuli za usafi wa mazingira ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Iringa ndiyo yenye bajeti ya asilimia 30 na Halmashauri nyingine zikiwa zimetenga chini ya asilimia 15. Changamoto nyingine ameitaja kuwa ni ongezeko la ujenzo holela wa makazi ya watu ambao hauendani na Sera ya Mipango Miji na kuifanya sekya ya Afya kushindwa kutoa huduma kamilifu katika maeneo yao.

Likangaga alizipongeza Halmashauri zilizoshinda katika mashindano hayo kitaifa na kuzitaja kuwa Manispaa ya Iringa ilikuwa mshindi wa pili kwa miaka mitatu mfululizo tokea mwaka 2008-2010. Mwaka 2010 Halmashauri tatu zilishiriki ambapo Njombe Mji ilikuwa mshindi wa kwanza, Halmashauri ya Wilaya Njombe mshindi wa kwanza na Manispaa ya Iringa mshindi wa pili.

Mashindano haya yalianza mwaka 2003 ambapo Halmashauri za Manispaa 12 na Jiji moja zilishiriki kama njia mojawapo ya kuhamasisha jamii juu ya umuhimu wa kuimarisha shughuli za usafi wa mazingira. Aidha, kuanzia mwaka 2005 mashindano haya yamekuwa yakijumuisha Halmashauri zote nchini.

No comments:

Post a Comment