CAG AZIAGIZA SEKRETARIATI ZA MIKOA KUSIMAMIA FEDHA ZA UMMA KATIKA HALMASHAURI
Na. Revocatus Kassimba, Ruvuma
Sekretariati za mikoa hapa nchini zimeagizwa kuzingatia Sheria,kanuni na taratibu za utumiaji wa fedha za serikali ili kuhakikisha Halmashauri zinapunguza hoja za ukaguzi wa Hesabu.
Agizo hilo limetolewa leo na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za serikali (CAG) Bw.Ludovick Utouh alipokuwa akiongea katika mkutano na viongozi wa serikali mkoani Ruvuma katika ukumbi wa Songea club.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw.Ludovick Utouh akiongea katika mkutano na viongozi wa serikali mkoani Ruvuma katika ukumbi wa Songea club.Kushoto ni Kaimu mkuu wa mkoa wa Ruvuma Kanali Mstaafu Edmund Mjengwa na kulia ni kaimu Katibu Tawala Mkoa Dkt Anselm Tarimo
Bw Utouh amesema kuwa licha ya udhaifu wa usimamizi wa sekeretariati za mikoa uliopo kuhusu Sheria kutokuweka wazi wazi mahusiano ya utendaji kazi kati ya Sekretariati za Mikoa na Halmashauri ni budi fedha za serikali zikasimamiwa kikamilifu na Maafisa Masuhuli wa Serikali katika mikoa
Aliongeza kusema licha ya Sekretariati za Mikoa kutokuwa na vitendea kazi na bajeti ya kutosha kwa ajili ya usimamizi wa Halmashauri hazimaanishi kuacha jukumu lake la kusimamia utekelezaji wa shughuli za Maendeleo katika halmashauri kwani fedha nyingi za serikali hupelekwa huko kusaidia wananchi.
“Wananchi wetu wengi wako vijijini na ndiko miradi mingi ya Maendeleo inakoelekezwa na serikali na kugharimia fedha nyingi hivyo ukaguzi na ufuatiliaji ni muhimu ukapewa kipaumbele na mikoa yote” alisema Bw Utouh
Aibainisha wazi kuwa Miradi mingi ya maendeleo inatekelezwa kwenye ngazi za uongozi za vijiji kulingana na sera ya D by D hivyo ufuatiliaji na tathmini ya thamani ya fedha ni muhimu hasa vijijini.
Bw .Utoh ametaja sababu zinazopelekea halmashauri nyingi hapa nchini kupata hati zisizoridhisha kutokana na fedha za serikali kutumika vibaya kuwa ni sheria za serikali za Mitaa kuwa za zamani hivyo kukinzana na Sheria zingine.
Aidha alitaja sababu zingine kuwa ni utaratibu wa kutuma fedha kwenye halmashauri kutokuwa na maelezo ya wazi na pia mfumo kutokuwa na utaratibu wa adhabu kwa wasiofikia Malengo yaliyowekwa.
Bw.Utouh amesema kuwa ukaguzi umebaini ya kuwa katika Mikoa mingi hapa nchini hakuna uhusiano mzuri wa utendaji kazi kati ya Sekretariati ya Mkoa, Halmashauri na Uongozi wa Vijiji hasa inapohusu usimamizi wa fedha na raslimali za umma.
Ili kutekelezan kwa makini usimamizi wa mapato na matumizi ya serikali mdhibiti na Mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali amewataka viongozi wa kisiasa kufuatilia taarifa zote za miradi ya Maendeleo na kuhoji matumizi ili uadhirifu wa fedha za umma ukome
Hata hivyo Bw Utouh ameaagiza wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuwawezesha waweka Hazina na Wahasibu wafundishwe juu ya viwango vya uhasibu vya kimataifa ili Kuboresha kazi zao itakazosaidia kupatikana kwa taarifa sahihi za Hesabu za Halmashauri .
No comments:
Post a Comment