Ofisi ya Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa (TANROADS) imekusanya zaidi ya shilingi milioni 18 katika kipindi cha kuanzia Julai, 2011 hadi Septemba, 2011 zikiwa ni tozo kwa magari yaliyozidisha uzito.
Taarifa hiyo imetolewa na Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa iringa, Mhandisi. Paul Lyakurwa, wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji kwa mwaka 2010/ 2011 na mpango wa matengenezo na ukarabati kwa mwaka 2011/2012 na taarifa ya utekelezaji hadi Septemba, 2011 ya Wakala wa Barabara Mkoa wa Iringa katika Kikao cha Bodi ya Barabara ya mkoa wa Iringa kilichofanyika katika ukumbi wa St. Dominic katika Manispaa ya Iringa,
Mhandisi. Lyakurwa amesema kuwa ofisi yake inajukumu la kudhibiti uzito wa magari barabarani kwa kutumia mizani isiyohamishika iliyopo Makambako.
Amesema katika kipindi cha Julai, 2011 hadi Septemba, 2011 magari yaliyopimwa ni 1,005 kati ya hayo magari 103 yalizidisha uzito na kulipishwa tozo la uharibifu wa barabara kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Barabara Na. 30 ya mwaka 1973 na kanuni zake za mwaka 2001 ofisi yake imekusanya shilingi 18.175 milioni.
Akielezea utekelezaji wa ahadi za Mhe. Dk. Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 zilizo katika Ilani ya uchaguzi ya CCM kuhusu sekta ya barabara Mkoani Iringa, hasa kukamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe- Makete (Km. 109 kwa kiwango cha lami amesema kuwa ujenzi wa Km. 11.5 kwa kiwango cha lami kati ya Mang’oto na Tandala ndani ya Wilaya ya Makete umekamilika kwa gharama ya shilingi 4,612,654 milioni.
Amesema ujenzi wa Km. 1 umepangwa kutekelezwa mwaka wa fedha 2011/2012 maeneo ya Mang’oto kwa gharama ya shilingi 797,040 milioni pamoja na utekelezaji huo kiasi cha shilingi 1,480,644 milioni zinahitajika kulipia deni la kazi zilizofanyika kati ya mwaka 2008/ 2009 na mwaka 2010/ 2011.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma ameagiza ushirikishwaji wa jamii katika utunzaji wa miundombinu ya Mkoa wa Iringa ili iweze kuwanufaisha wananchi walio wengi.
Akifungua kikao cha Bodi ya Barabara cha Mkoa wa Iringa, amesema bado kuna mapungufu kadhaa katika ushirikishwaji wa jamii katika utunzaji wa miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Iringa hususani shughuli zinazofanyika ndani ya hifadhi ya barabara na kuagiza jamii ihusishwe kikamilifu katika utunzaji huo wa miundombinu ya barabara.
=30=
No comments:
Post a Comment