Saturday, December 17, 2011


Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Gertrude Mpaka ameshauri kudumisha ushirikiano wa kimkakati baina ya watumishi wa serikali na sekta binafsi ili jitihada za kumletea maendeleo mwananchi ziendelee kuzaa matunda mara dufu.
Mpaka amesema hayo katika mahojiano maalumu na gazeti la Mwananchi alipokuwa akiwasili katika viwanja vya maonesho vya Mwalimu Julius Nyerere jijini hapa.
Amesema, “mafanikio katika utumishi wa Umma yataletwa kwa kudumisha ushirikiano baina ya watumishi wa Umma na watumishi wa Umma, na watumishi wa Umma na taasisi nyingine zisizo za Umma”. Amesema, “ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu ya kiserikali ndio msingi wa mafanikio na hasa umuhimu huo huonekana pale unapotumika katika kutatua changamoto inayoikabili taasisi na kutafutiwa ufumbuzi wake kwa kuusisha mtumishi zaidi ya mmoja kwa maana nyingine uhumihu huo kufanya kazi kwa umoja”.
Mpaka amesema kuwa Mkoa wa Iringa umefanikiwa katika miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kutokana na dhana ya ushirikiano na umoja katika utendaji kazi.  Amesema, sekta za afya, elimu, miundombinu, maji na utawala bora katika Mkoa wa Iringa zimefanikiwa kwa kiwango kikubwa kutokana na ushirikiano huo.
Akiongelea utawala bora, amesema Mkoa umeendelea kuweka masanduku ya maoni katika sehemu zote za kutolea huduma kwa lengo la kuboresha utoaji huduma kwa kuwapa wananchi nafasi ya kutoa maoni, malalamiko na michango yao kwa lengo la kuusaidia Mkoa katika kuzitatua kero hizo. Ameongeza kuwa Ofisi yake inae Afisa anayeshughulikia pamoja na mambo mengine malalamiko ya wananchi na watumishi na utaratibu huo umeteremshwa hadi katika Ofisi za Wakuu wa Wilaya na Tarafa.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, amesema utawala bora katika ngazi ya Mkoa umejikita pia katika uboreshaji wa ofisi za Tarafa ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Amezitaja ofisi 14 za Tarafa zilizojengwa katika uboreshaji na usogezaji wa huduma karibu na wananchi kuwa ni Pawaga, Liganga, mwambao, Masasi, kalenga, Mlolo, Ifwagi, kibengu, Makambako, Magoma, Ukwama, Ikuwo, Malangali na Mahenge. Amesema zaidi ya lengo la kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi pia Mkoa umelenga kuyaboresha mazingira ya kazi ya Maafisa Tarafa.
Amesema, Mkoa umeendelea kutumia mbinu ya fursa na vikwazo vya maendeleo (o & OD) na inayowahusisha wadau wengine wa maendeleo hutumika katika kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya kijiji.
Atuganile George ni miongoni mwa wananchi waliofika kutembelea mabanda ya maonesho katika viwanja vya mwalimu Julius Nyerere amesema kuwa katika miaka ya hivi karibuni sekta ya Utumishi wa Umma imeendelea kuboreka tofauti na kipindi cha nyuma. Amesema “unajua ndugu mwandishi kipindi hiki hata ukiingia katika baadhi ya ofisi za serikali unajisikia kuwa umeingia katika ofisi zinazotoa huduma kwa wananchi kiukweli hali imebadilika na kuwa bora”.
=30=

No comments:

Post a Comment