Saturday, December 17, 2011

MIAKA 50 NI MAFANIKIO NA CHANGAMOTO


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka watanzania kuyatumia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa kutafakari mafanikio na changamoto kama taifa kwa kufanya ulinganifu na uchambuzi kupitia taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali nchini.
Kauli hiyo ameitoa nje ya banda la Mkoa wa Iringa, alipofanya ziara ya kujifunza mafanikio na changamoto za miaka 50 ya Uhuru katika viwanja vya maonesho ya maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara vya Mwalimu Julius Nyerere.
Mkuu huyo  wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru ni maadhimisho maalumu, tofauti na sherehe za maadhimisho tulizozoea kufanya kutokana na uzito wa kimantiki kupitia madhumuni na kaulimbiu ya maadhimisho hayo isemayo “tumethubutu, tumeweza na tunazidi kusonga mbele”.
Amesema kwa upande wake anakubaliana kimsingi na hatua ya serikali ya kuamua kuhadhimisha maadhimisho hayo kwa kuzihusisha taasisi mbalimbali nchini katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere ili kuwapatia wananchi fursa ya kujionea na kupata maelezo ya kina juu ya maendelea yaliyopatikana katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo. Amesema, “zaidi ya wananchi hata watendaji wa serikali lazima wayatumie maadhimisho hayo kubadilishana uzoefu na mbinu za kukabiliana na changamoto katika baadhi ya maeneo ambayo taasisi nyingine zimefanya vizuri zaidi, na hii ndiyo maana ya maadhimisho yenyewe ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara”.
Akiongelea mafanikio ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa Mkoa wake wa Iringa, Dk. Christine amesema kuwa kama Mkoa pamoja na mambo mengine, anajivunia kuongezeka kwa pato la Mkoa. Amesema, “ukirejea kipindi cha Uhuru, pato la Mkoa wa Iringa lilikuwa ni shilingi 5,693,000, wakati wastani wa pato la mkazi likiwa ni shilingi 103.  Katika mwaka 2010 pato la Mkoa wa Iringa liliongezeka hadi kufikia shilingi 1,702,430,000, wakati pato la mkazi nalo liliongezeka hadi kufikia shilingi 979,882”.
Amesema changamoto anayoiona kwa sasa ni kulitafsiri pato hilo kwa maana ya mkazi mmoja mmoja na jinsi linavyochangia katika kubadilisha maisha yake ya kila siku badala ya kuonekana katika ujumla wake. Akifafanua zaidi amesema kuwa sehemu kubwa ya pato la Mkoa wake huchangiwa na mashamba makubwa ya chai  na viwanda vya chai, misitu na viwanda vya mbao na tumbaku.
Ukiwa umesheheni wataalamu wa fani kadhaa, Mkoa wa Iringa unaokadiriwa kuwa na wakazi 1,764,285 pamoja na Halmashauri zake ni miongoni mwa taasisi za serikali zinazoshiriki katika maadhimisho hayo, ukiwa unashiriki kikamilifu katika kuonesha, kuchangia uzoefu wa mafanikio, changamoto na wadau mbalimbali nchini.
=30=

No comments:

Post a Comment