Saturday, December 17, 2011

WALIMU WA KUJITOLEA WASAIDIWE


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amezishauri serikali za kata na vijiji kuangalia uwezekano wa kuwasaidia vijana wanaofanya kazi ya kufundisha kwa kujitolea baada ya kumaliza masomo yao.
Ushauri huo ameutoa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa kata ya Idunda iliyopo wilayani Mufindi.
Mkuu wa Mkoa alikuwa akijibu swali juu ya mpango wa serikali wa kuwaajiri vijana wanaojitolea kufundisha katika shule za msingi na sekondari  katika baadhi ya maeneo ya Wilaya ya Mufindi. Dk. Ishengoma amesema “ni kweli vijana hawa wanaokuwa wamemaliza kidato cha nne na sita na kujitolea kufundisha madarasa yaliyochini  yao wanamchango mkubwa katika kutoa mchango wao kwa kuwafundisha wananfunzi wa shule za msingi na sekondari”.
 Amesema kutokana na upungufu wa walimu uliopo katika baadhi ya maeneo ya Kata za Wilaya ya Mufindi, vijana hawa wanaojitolea wanasaidia kupunguza upungufu uliopo ila ni jukumu la serikali za vijiji na kata iangalie upungufu uliopo katika ikama za shule zao na kuweka mikakati ya kuwasaidia ili wanafunzi waweze hao wakati serikali inaendelea kuongeza idadi ya walimu katika shule zake.
Aidha, kuhusu kuwaajiri amesema kuwa serikali haina utaratibu wa kuwaajiri watumishi wasiopitia mafunzo na kupata utaalamu unaostahili katika fani husika. Mkuu wa Mkoa ameziagiza Hamlashauri pindi yanapotokea matangazo ya kozi mbalimbali yaweze kutawanywa katika Kata na vijiji ili vijana wengi waweze kuyasoma na kuomba kozi hizo.
Akiongelea changamoto inayoikabili shule ya sekondari ya Idunda sambamba na umbali wa wanafunzi kati ya nyumbani na shuleni, Dk. Ishengoma amewataka wananchi wa Kata hiyo kuanza ujenzi wa Daharia za wanafunzi kwa juhudi na kuahidi kuwachangia shilingi 1,000,000. 
=30=

No comments:

Post a Comment