Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru hayawezi kutenganishwa na juhuri zilizofanywa na Baba wa Taifa katika kupigania Uhuru wa Tanzania na hapo ndipo historia inapoanzia.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amesema kuwa tupo hapa leo kwa ajili ya kuadhimisha maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika katika Tarafa ya Mdandu wilayani Njombe. Kwa ujumla Mwaka huu una umuhimu wa kipekee hasa kwa Historia ya nchi yetu. Hapa tulipofika na hatua tuliyopiga sio ya kubezwa hata kidogo kama baadhi ya watu wanavyotaka tuamini kuwa hakuna chochote kilichofanyika katika kipindi hiki cha miaka 50 ya Uhuru.
Dk. Ishengoma amesema “Sio rahisi kusherehekea Miaka 50 ya Uhuru bila kukumbuka juhudi zilizofanywa na Baba wa Taifa na Muasisi wa Chama cha TANU katika harakati za kupigania Uhuru”. Amesema “Nchi yetu ilikuwa duni sana wakati wa uhuru kutokana na ujenzi wa mfumo wa Ubepari, Ukabaila na Unyonyaji ilivyokuwa imejengwa wakati huo”.
Dk. Ishengoma amesema ili kuinusu nchi hii zilihitajika juhudi zenye dhamira ya kizalendo zilizofanyika kupitia Azimio la Arusha, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, Siasa ni Kilimo, ‘Operatio’ vijiji, kisomo chenye manufaa, kuunganishwa kwa TANU na ASP na kuzaliwa kwa CCM, kurejeshwa kwa serikali za mitaa na kung’atuka kwa viongozi kwa mujibu wa Katiba.
Amefafanua kuwa haya yote mafanikio makubwa nchi inayojivunia kwa miaka 50 ya Uhuru misingi yake imejengwa katika uzalendo huo.
Akiongelea mafanikio ya elimu, amesema “Tulipopata uhuru, kilikuwepo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam tu kilichokuwa na wanafunzi 14 wa kitivo cha Sheria. Sasa Tanzania ina vyuo vikuu na vyuo vishiriki visivyopungua 30. Mkoa wa Iringa Peke yake tuna Vyuo Vikuu 5”. Haya ni mafanikio makubwa sana na si ya kubeza hata kidogo.
Mkoa wa Iringa ukiwa ni miongoni mwa mikoa ya Tanzania Bara unaadhimisha miaka 50 ya Uhuru sambamba ya maonesho ya shughuli mbalimbali zinazofanyika katika Mkoa huo chini ya kauli mbiu “tumethubutu, tumeweza na tunazidi kusonga mbele”. Aidha, mkoa huo umepangiwa kufanya maadhimisho hayo tarehe 7-9 Novemba mwaka huu.
=30=
No comments:
Post a Comment