Saturday, December 17, 2011

MALENGAMAKALI WEKEZENI KATIKA ELIMU


Mkuu wa Mkoa wa Iringa amewataka wananchi wa kata ya Malengamakali kuwekeza katika elimu ya watoto wao ili iweze kuwasaidia kwa kujiletea maendeleo.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa kata ya Malengamakali iliyopo katika Jimbo la Ismani katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Dk, Ishengoma amesema “kwa kuwa leo tumepata nafasi ya kukutana hapa napenda kuwaomba wazazi wote kuhakikisha watoto wote waliomaliza darasa la saba na kufaulu wanahimizwa kwenda sekondari”.  Amesema elimu ndiyo hazina pekee mzazi anayoweza kujivunia kwa mtoto wake hivyo ni lazima kuhakikisha watoto wote waliofaulu wanapelekwa sekondari.
Kwa upande wa kilimo Mkuu wa Mkoa amesema kuwa kutokana na sehemu kubwa ya Mkoa kukumbwa na upungufu wa chakula uliosababishwa na upungufu wa mvua ulioleteleza ukame, mkoa umeweka mkakati wa kilimo cha mazao yanayostahimili ukame. Amesama mkakati unaoendelea kwa sasa ni kilimo cha zao la mtama.
Amesema kwa sasa wananchi wa mkoa wa Iringa tunaimba wimbo mmoja nao ni kilimo cha mtama. “Tumekubaliana kilimo cha zao la mtama kwa sababu zao la mtama linavumilia ukame kutokana na upungufu wa mvua”.  Amesema “pamoja na shukrani tunazozitoa kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano kutupatia chakula cha njaa, lakini hatuwezi kukubali kama wanairinga huo ukawa utaratibu wetu wa kusaidiwa chakula cha njaa, lazima sisi wenyewe kukabiliana kwa pamoja na upungufu wa chakula kwa kulima mazao yanayovumilia ukame”.
=30=

No comments:

Post a Comment