Saturday, December 17, 2011

IRINGA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA MAWASILIANO


Mkoa wa Iringa umeendelea kuimarisha sekta ya miundombinu ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wake wananufaika zaidi na miundombinu hiyo kwa kujiletea maendelea endelevu.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma katika hotuba yake ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara katika Mkoa wa Iringa yanayofanyika katika Tarafa ya Mdandu Wilayani Njombe.
Dk. Christine amesema “mwaka 1961 hali ya miundombinu ya mawasiliano katika Mkoa wa Iringa ilikuwa duni sana, barabara nyingi zilikuwa hazipitiki kwa urahisi kwa mfano kwenda Ludewa au Makete tulitumia siku 2 au 3”.
Amesema mwaka 1961 mkoa wa Iringa ulikuwa na mtandano wa barabara upatao Km. 1,209.5 kati ya hizo Km. 76 ni barabara za vumbi na Km. 1,133.5 ni changarawe. Mwaka 2010 mtandao huo umeongezeka hadi kufikia Km. 8,776.56 kati ya hizo Km. 530.1 ni lami, Km. 5,942.06 ni changarawe na Km. 2,304.40 ni barabara ya udongo.  
Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameeleza mafanikio makubwa katika mawasiliano ya simu za mkononi, redio, televisheni, mtandao wa interneti, magazeti na fax. Ameongeza kuwa Mkoa umefanikiwa kuwa na umeme katika makao makuu ya wilaya zote.
Aidha, amesema kuwa ili Mkoa wa Iringa uendelee kupata mafanikio makubwa katika Nyanja za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ni lazima kudumisha amani iliyoachwa na waasisi wa taifa letu. Amesema kuwa kudumisha amani, utulivu na mshikamano ni njia pekee ya kuwaenzi waasisi wa taifa letu.
Katika taarifa fupi ya Wilaya ya Njombe, iliyowasilishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Sara Dumba, amesema kuwa wilaya yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika sekta ya elimu ndani ya miaka 50 ya Uhuru. Amesema katika elimu ya msingi wilaya imeweza kuongeza idadi ya shule toka shule za msingi 44 hadi kufikia shule 260. Amesema kuwa shule za sekondari pia zimeongezeka kutoka moja mwaka 1971 hadi kufikia shule 62 mwaka 2011. katika elimu ya ufundi, wilaya ilikuwa na shule na vituo vya ufundi stadi vinne wakati wa uhuru lakini kufikia mwaka 2011 vimeongezeka hadi kufikia 12.
Sara amesema kuwa sekta ya afya nayo haikubali nyuma, mwaka 1961 wilaya yake ilikuwa na hospitali moja na kufikia sasa wilaya ina hospitali tatu, vituo vya afya vipo 11, zahanati zipo 99. Amesema kuwa wilaya yake inajivunia sekta hiyo kuendelea kutoa huduma nzuri na chanjo kwa magonjwa mbalimbali kwa mama wajawazito na watoto.

No comments:

Post a Comment