Saturday, December 17, 2011

IDODI FIKIRIENI KILIMO CHA MTAMA


Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa Tarafa ya Idodi kufikiria kilimo cha mazao yanayostahimili ukame ili kukabiliana na tatizo la njaa linalowakabili wananchi wa Tarafa hiyo mara kwa mara.
Dk. Ishengoma anayefanya ziara maalumu ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu katika Mkoa wa Iringa, siku yake ya kwanza ya ziara aliyoifanya katika Kata ya Nzihi, Tungamalenga na Mahuninga amesisitiza kilimo cha zao la mtama pamoja na mazao mengine. Amesema “si lazima kulima mahindi na mpunga tu kama zao la chakula, bali tubadilishe kidogo fikra ili tuweze kulima mazao yanayostahimili ukame na tuanze na zao la mtama”.
Amesema pamoja na jitihada za Serikali ya Mkoa kuhimiza kilimo cha zao la mtama lakini mkulima mmoja mmoja ni vizuri akalima pia muhogo na viazi vitamu kwa kujihakikishia uhakika na hifadhi ya chakula.
Amesema kuwa matarajio ni kila kaya kulima angalau ekari mbili za mtama. Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, itazigawa hizo mbegu bure kwa wakulima na kuwakumbusha wakulima kuwa wamebakiwa na kazi moja tu ya kulima baada ya kuondolewa gharama za kununua mbegu ya mtama. Vilevile, amesisitiza kuwa serikali itakuwa makini katika kuzigawa mbegu hizo kwa kuangalia eneo lililolimwa ili kuepukana na baadhi ya wakulima kuzitumia kwa matumizi mengine tofauti na makusudio yaliyokusudiwa na serikali.
Aidha, amewataka wananchi kujihusisha na ufugaji wa wanyama wadogo wadogo ili uweze kuwasidia katika kukidhi mahitaji ya kawaida ya nyumbani. Amesema “ufugaji wa wanyama wadogowadogo unasaidia sana hasa akina mama kuweza kukidhi mahitaji ya familia”.
Akiongelea ufugaji wa ng’ombe ameshauri kuwa yatumike madume bora ili kupata maziwa mengi. Vilevile ameshauri kutumia njia ya uhamilishaji ili kupunguza gharama za ufugaji wa madume mengi ya ng’ombe na uhifadhi wa mazingira.
Kuhusu elimu, Mkuu wa Mkoa ameagiza watoto wote watakaofaulu wapelekwe shule ili kukuza kuwango cha elimu katika Mkoa. Amesema “kila mmoja lazima aone fahari kumpeleka mwanae shule na hasa watoto wa kike ili kuachana na tamaduni za kale zilizokuwa zikimfanya mtoto wa kike kukosa elimu”.
=30=

No comments:

Post a Comment