Saturday, December 17, 2011

RC AKEMEA UKATAJI MITI


Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameagiza kuacha tabia ya kukata miti ovyo ili kuunusuru Mkoa na kugeuka jangwa kama baadhi ya maeneo ambayo yanakubwa na ukame wa mara kwa mara na kusababisha upungufu wa chakula.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma wakati akiongea na wananchi wa Kata ya Idodi iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa alipofanya ziara ya kuhamasisha shughuli za kilimo na elimu.
Dk. Ishengoma amesema kuwa katika kipindi cha kuandaa mashamba wananchi wamekuwa na tabia ya kukata miti katika mashamba yao. Amesema “msikate miti yote sababu miti hii ndiyo inayotengeneza mvua hivyo, tukiendelea kukata miti hiyo ukame hautaisha bali utazidi kuongezeka katika eneo kubwa zaidi”.
Kutokana na ukame wa mara kwa mara unaosababisha upungufu wa chakula, Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na upungufu wa chakula ikiwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha mtama amesema Dk. Ishengoma.
Amesema ni vizuri wananchi wakabadili mawazo ya kutegemea mazao ya mahindi na mpunga pekee na kufikiria kilimo cha zao la mtama.
Akiongelea vocha za pembejeo za kilimo, amesema kuwa wananchi waliopata vocha hizo wazitumie vizuri ili kuweza kunufaika nazo na kufikiwa kwa malengo ya serikali ya kuwainua wananchi kiuchumi kupitia kilimo. Amesema wananchi wanawajibu wa kufahamu kuwa seti moja ya vocha za pembejeo inahusisha mbolea ya kupandia, mbegu bora na mbolea ya kukuzia.
Aidha, alitahadharisha kwa mawakala wasiowaaminifu kuwa lazima wafuate utaratibu uliowekwa katika usambazaji na matumizi ya vocha hizo na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wakala yeyote atakayekiuka utaratibu uliowekwa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa anafanya ziara ya kuhamasisha kilimo na elimu baada ya msimu wa kilimo kuanza wakati baadhi ya sehemu katika Tarafa ya Idodi ni miongoni mwa maeneo yaliyokubwa na ukame na kusababisha upungufu mkubwa wa chakula. 
=30=

No comments:

Post a Comment