Wednesday, February 15, 2012

Mgodi wa Tarajali kuanza Ruvuma

Na. Revocatus Kassimba, Ruvuma
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Mohamed Ghalib Bilal amewahakikishia wakazi wa Mkoa wa Ruvuma na Tanzania kwa ujumla kuwa  mradi wa mgodi tarajali wa Urani wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma utatekelezwa kwani una umuhimu na maslahi kitaifa.

 Makamu Rais Dk. Mohamed Ghalib Bilal akihutubia mamia ya wananchi wa kijiji cha Likuyu Sekamaganga wilaya ya Namtumbo wakati alipofanya ziara katika mradi wa urani

Dk. Bilal amesema hayo wakati akiongea na wafanyakazi wa mgodi huo unaomilikiwa na kampuni ya Mantra Tanzania kuwa Serikali inafuatilia kwa makini kuona madini hayo muhimu yanalifaidisha Taifa.

Aliongeza kuwa anao uhakika kuwa taratibu zote za hifadhi ya mazingira na usalama wa maisha ya wakazi wanaozunguka eneo hilo umetiliwa mkazo na kampuni kwa kushirikiana na taasisi ya nishati ya atomiki nchini.

Aidha, kwa upande wake Mkurugenzi wa Mantra Tanzania, Asa Mwaipopo ameiomba Serikali kuharakisha taratibu za kisheria ili mgodi uweze kuanza hapo mwaka ujao kwa ujenzi na ifikiapo 2014 uzalishaji uanzae ili ajira zipatazo 1600 wakati wa ujenzi wa mgodi na nyingine 400 wakati wa uzalishaji ziweze kupatikana kwa watanzania na kusaidia kukuza uchumi.

 
Makamu wa Rais akipokewa na viongozi wa kampuni ya Mantra wakati alipowasili katika eneo litakalojengwa mgodi wa Uranium wilaya ya Namtumbo


Monday, February 6, 2012

Ruvuma na Cuba


Na. Revocatus Kassimba, Songea
Serikali mkoani Ruvuma imeihakikishia nchi ya Cuba kuendeleza ushirikiano  ili kuboresha mahusiano mema yaliyojengeka kwa miongo zaidi ya minne hususan katika kuendeleza huduma za afya nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo mjini Songea na Kaimu Katibu Tawala  Mkoa wa Ruvuma  Dkt Anselm Tarimo alipokuwa akiongea na Balozi wa Cuba nchini Ernesto Gomez Diaz alipofanya mazungumzo na uongozi wa Sekretariati ya Mkoa wa Ruvuma.
Dkt Tarimo alielezea Uhusiano wa kiurafiki uliopo na nchi ya Cuba kuwa umesaidia sana katika jitihada za serikali ya Tanzania kuwapatia wananchi wake Huduma bora  na za uhakika za afya.
Alisema kwa kipindi kirefu nchi ya Cuba imekuwa ikisaidia Tanzania kwa kuipatia wataalam wa afya hususan madaktari wanaofanya kazi katika hospitali mbalimbali nchini ambapo katika mkoa wa Ruvuma wapo madaktari wawili kutoka nchini Cuba.
“Tunashukuru kwa ushirikiano tulionao baina ya nchiz zetu mbili kwani kuanzia miaka ya 1980 mkoa wetu umekuwa ukipokea madaktari kutoka nchini Cuba ambao wanasaidia kutoa Huduma za tiba katika hospitali yetu ya Mkoa Songea” alisema Dkt Tarimo
Aliongeza kusema kwa sasa mahitaji ya madaktari ni makubwa kutokana na hospitali ya mkoa kupandishwa hadhi na kuwa ya rufaa hivyo ni vema Cuba ikaongeza wataalam zaidi
Naye Balozi wa Cuba nchini Ernesto Gomez Diaz alishukuru serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Jakaya Kikwete kwa kuendeleza na kudumisha ushirikiano kati ya nchi zote mbili  toka enzi za waasisi  Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania na Fidel Castro wa Cuba
Balozi Diaz amesema Cuba ni nchi pekee iliyobaki inayofuata mfumo wa Ukoministi  Duniani wenye lengo la kuhakikisha maisha ya kijamaa ambapo rasilimali za umma zinatumika kwa wote
Aliongeza kusema kuwa katika nchi ya Cuba kutokana na sera ya Ukoministi serikali imefanikiwa kutoa Huduma za afya na Elimu bure kwa raia wake wote na kusema kuwa nchi yake itaendelea kutoa kipaumbele kwa watanzania kwenda kusoma udaktari nchini Cuba .
Balozi Diaz yupo mkoani Ruvuma kwa ziara ya kikazi ya siku mbili ambapo amepata fursa ya kutembelea na kukagua Hospitali ya mkoa ambapo nchi yake ina madaktari wawili wanaofanya kazi.
Ameshukuru uongozi wa serikali kwa kutoa ushirikiano kwa wataalam hao wa Cuba kwa kipindi chote wanachofanya kazi kwani wameendelea kufurahi uwepo wao hapa mkoani.

...RUVUMA WATAKIWA KULIMA MAHINDI KWA WINGI

Na. Revocatus Kassimba, SONGEA
Serikali imewataka wakulima  mkoani Ruvuma kulima kwa wingi mahindi katika msimu huu kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo licha ya changamoto za soko lililowakabiri msimu wa kilimo uliopita.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Said Thabit Mwambungu wakati wa ziara yake katika vijiji vya Magagula, Lugagala na Muungano Zomba vilivyopo wilaya ya Songea .
Mwambungu aliwaeleza wananchi kuwa serikali inatambua kero ya ununuzi wa mahindi iliyotokea msimu wa 2011/2012 ambapo wakulima wengi walichelewa kupokea fedha zao kutoka Wakala wa Hifadhi za Chakula (NFRA).
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu (mwenye kaunda suti nyeusi) akisikiliza maelezo ya kilimo kutoka kwa Mkuu wa wilaya ya Songea, Thomas Sabaya (kulia) wakati wa ziara ya kukagua usambazaji wa pembejeo za kilimo katika kijiji cha Lugagara wilaya ya Songea
Aliongeza kusema kuwa changamoto ya fedha za wakulima hazitajitokeza tena msimu ujao kwani tayari serikali imejiandaa kwa kutengwa fedha katika bajeti ili kuhakikisha mahindi yote yatanunuliwa kwa wakati.
“Limeni kuliko mwaka jana kwani serikali imejipanga kununua kwa wakati na kuhakikisha kuwa hakuna mkulima atakayecheleweshewa malipo na serikali” alisema Mwambungu na kuongeza kuwa hakuna mkulima sasa anayeidai serikali wote wamelipwa.
Mkuu wa mkoa Mwambungu alisisitiza kuwa serikali inafanya kila linalowezekana kuondoa kero ya kukopa mahindi ya wakulima hivyo ni vema wakulima wakaendelea kuunga mkono juhudi hizi za serikali kwa kuongeza uzalishaji.
Katika msimu 2011/2012 wa kilimo kwa mujibu wa taarifa za Wakala wa Hifadhi ya Chakula jumla ya tani 50,018 za mahindi zimenunuliwa kutoka kwa wakulima mkoani Ruvuma zenye thamani ya shilingi bilioni 17.5 ambapo kilo ilinunuliwa kwa shilingi 350.
Mkuu wa Mkoa alitumia fursa hiyo kuwapongeza wakulima wa vijiji hivyo alivyovitembelea kwa kutumia vema pembejeo za ruzuku kwa mfumo wa vocha kwani wameongeza uzalishaji wa mahindi na kuifanya wilaya ya Songea kuongoza katika kuzalisha mahindi mkoani.
Ziara ya Mkuu wa mkoa ilihusisha pia kukagua zoezi la ugawaji wa vocha za pembejeo ambapo kwa mujibu wa taarifa ya iliyotolewa na Mkuu wa wilaya ya Songea Thomas Sabaya alisema wilaya imepata mgao wa vocha 64,417 ambazo zimesambazwa kwa wakulima.

Wakulima wa kijiji cha Magagula Wilaya ya Songea wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu (hayupo pichani) jana alipofanya ziara ya kukagua shughuli za kilimo
Kuhusu mbolea ya kukuzia (UREA) mfuko unauzwa shilingi 72,000/= na mkulima anachangia shilingi 52,000/= huku serikali ikilipia zinazobaki na kwa mbegu bora mfuko unauzwa shilingi 40,000/= huku mkulima akichangia 20,000/= na serikali zinazobakia.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kijiji cha Lugagara Bi Taifa Mahundi katika risala yake alisema wakulima wana changamoto kubwa ya upungufu wa vocha za ruzuku hivyo akaiomba serikali kuongeza mgao kwa kijiji.
Mkuu wa mkoa akijibu hoja hiyo aliwafahamisha wananchi kuwa vocha zinazotolewa ni vigumu kufanana na idadi ya wakulima kwani hiyo ni ruzuku itolewayo na serikali kuwasaidia wakulima kujenga uwezo wa kujitegemea.
Katika msimu huu wa kilimo mkoa wa Ruvuma umepatiwa vocha za ruzuku ya pembejeo za kilimo 192,000 ambapo kwa mwaka uliopita ulipatiwa vocha 204,000 hivyo kuwa na upungufu wa vocha 12,000/=.
Mkoa wa Ruvuma ni kati ya mikoa sita maarufu kwa uzalishaji wa mahindi nchini ambapo mikoa mingine ni Iringa, Mbeya, Rukwa, Kigoma na Morogoro.
Sabaya alisema vocha hizo zinahusisha mbegu bora za mahindi, mbolea ya kupandia na mbolea ya kukuzia ambapo bei ya mfuko wa mbolea ya kupandia (DAP) inauzwa shilingi 80,000/=huku mkulima akichangia shilingi 52,000/=.