Mkuu wa Mkoa wa Iringa ametoa wito
kwa viongozi wa mkoa wake kutoa ushirikiano wa kutosha kwa mamlaka ya
uendelezaji wa bonde la mto Rufiji (RUBADA) ili kuwawezesha kuratibu na
kusimamia vizuri mipango kabanbe ya kuendeleza shughuliza kilimo kwa ukanda wa
kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Katika hotuba ya ufunguzi wa kikao
cha viongozi na wataalamu wa mkoa wa Iringa kuhusu uendelezaji wa SAGCOT
uliofanyika katika ukumbi wa VETA mjini Iringa iliyosomwa na Mkuu wa Wilaya ya
Kilolo, Gerald Guninita kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Christine
Ishengoma.
Mgeni rasmi Gerald Guninita ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Kilolo (katikati) akisoma hotuba wakati wa ufunguzi wa kikao cha viongozi na wataalamu wa mkoa wa Iringa kuhusu uendelezaji wa SAGCOT
wajumbe wa kikao cha viongozi na wataalamu wa mkoa wa Iringa kuhusu uendelezaji wa wa SAGCOT
Amesema RUBADA imepewa majukumu ya
kusimamia na kuratibu mipango ya SAGCOT ili malengo ya mipango hiyo yaweze
kutekelezwa vizuri na kuinua hali ya wananchi nchini. Amesema katika kufanikisha
hili RUBADA inatafuta na kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo chenye
tija na viwanda kwa lengo la kuleta mapinduzi ya kijani. Amesema katika hilo
RUBADA kwa kushirikiana na wilaya husika itaandaa mipango ya matumizi bora ya
ardhi ya vijiji ili maeneo ya uwekezaji yabainishwe na kutengwa kwa ajili ya
wawekezaji watakayoyaendeleza pamoja na wakulima wadogo wadogo wanaoyazunguka
maeneo ya miradi hiyo.
Guninita amesema kwa kuzingatia kazi
nzuri inayofanywa na RUBADA katika kutekeleza mipango hiyo, ushirikiano wa
viongozi na wataalamu hao ni chachu katika ufanikishaji wa malengo hayo.
Ameelezea matarajio yake kwa viongozi na wataalamu hao baada ya kikao hicho
kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kuwaelimisha wananchi katika maeneo yao ili
wawe washiriki wazuri katika kutekeleza mpango huo.
Akiwasilisha mpango wa SAGCOT
Mkurugenzi Mkuu wa uendeshaji wa bonde la Rufiji, Aloyce Masanja amesema kuwa
hakuna nchi iliyofanikiwa duniani kuichumi na kuondokana na umasikini pasipo
mapinduzi ya kilimo na viwanda. Akiongelea takwimu, amesema kuwa asilimia 65 ya
malighafi za viwanda zinatokana na kilimo wakati asilimia zaidi ya 55 ya
mfumuko wa bei huchangiwa na mazao ya kilimo. Amesema katika hekta milioni 44
zinazofaa kwa kilimo ni asilimia 23 pekee ndiyo zimetumika.
Akiongelea tofauti kati ya kilimo
kwanza na sera nyingine zilizopita, Masanja amesema kuwa mipango na jitihada za
zamani ziliibuliwa, kupangwa na kutekelezwa na serikali na mashirika yake
pasipo kuwahusisha wadau wengine kikamilifu. Amesema tofauti na mipango ya
awali kilimo kwanza ni mtazamo mpana wa mabadiliko ya kisekta na uzoefu
uliopatikana kutokana na mipango iliyotekelezwa hapo awali na sasa kilimo
kwanza kimeshirikisha wadau wote.
Mkurugenzi Mkuu wa uendeshaji wa
bonde la Rufiji ameyataja malengo ya SAGCOT kuwa ni kutatua matatizo
yanayoikabili sekta ya kilimo hasa upatikanaji wa mitaji, vyama vya wakulima,
miundombinu ya kilimo, uharibifu wa mazingira, ukosefu wa masoko, uwekezaji
mdogo katika kilimo na uboreshaji wa sera zinazohusu kilimo. Amesema malengo
mengine ni kuwahamasisha wakulima wadogo na kuwaunganisha katika vikundi na
kuwafanya walime kilimo cha kibiashara.
Masanja amesema kuwa RUBADA imekuwa
pia ikiwapa kipaumbele vijana katika shughuli mbalimbali za kujiongezea kipato.
Amesema “kila tunapoanzisha miradi ya RUBADA tunakuwa tukianzisha kambi za
vijana ambapo tunawafundisha mbinu bora za kilimo na matumizi ya dhana za
kilimo” amesisitiza Masanja.
=30=
No comments:
Post a Comment