Hospitali ya Aga
Khan imefanikia kuanzisha huduma ya kuboresha afya ya mama mjamzito na mtoto
kwa kupitia mradi wake wa Tuunganishe mikono pamoja na mwanamke wa kwanza mjamzito
amefanikiwa kujifungua salama asubuhi ya leo.
Akizungumza na
waandishi wa habari muda mfupi baada ya kukabidhi zawadi kwa niaba ya jamuiya
ya Aga Khan mkoa wa Iringa, Meneja wa hospitali ya Aga Khan-Iringa, Veronica
James amesema “leo imekuwa ni siku ya furaha sana kwa hospitali ya Aga Khan na
kwa wananchi wa manispaa ya Iringa na vitongoji vyake kutokana na huduma za
kujifungua kwa mama mjamzito wa kwanza hospitalini hapa”.
Akielezea
malengo ya mradi wa Tuunganishe nikono pamoja Veronica amesema kuwa mradi huo
unalenga kuwasogezea wananchi huduma karibu na kwa ubora unaotakiwa kwa
kupunguza foleni kwa wanawake wajawazito katika vituo vingine vinavyotoa huduma
ya mama wajawazito na kujifungua kwa lengo la kuwapunguzia hadha wajawazito hao.
Meneja wa
hospitali ya Aga Khan iringa amesema kuwa mradi huo unalenga kuongeza kiwango
na matumizi ya huduma ya afya ya mama mjamzito na watoto nchini. Amesema kuwa
mradi huo pia unalenga kuboresha kiwango cha upatikanaji wa huduma ya afya ya
mama mjamzito na watoto. Malengo mengine ameyataja kuwa ni pamoja na kuboresha huduma
ya afya yam ma mjamzito na watoto katika jamii na kushirikiana na kujifunza
kuhusu afya ya mama mjamzito na watoto.
Akielezea furaha
yake mama mzazi Kerstin Scheffler (38) amesema kuwa amefurahishwa na huduma
katika hospitali hiyo kwa kipindi chote alichokuwa hospitalini hapo kutoka kwa
madaktari na wauguzi. Mama huyo aliyejifungua mtoto wake wa tatu leo na kupewa
jina la Malaika Lina ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuzitumia huduma za
afya ya mama mjamzito na mtoto katika hospitali hiyo ili waweze kunufaika
vizuri.
Katika maelezo
yake ya jumla Daktari mfawidhi wa hospitali ya Aga Khan Iringa, Dkt. Jumaa Mbete amesema mama huyo
amejifungua salama majira ya saa 3:25 asubuhi hospitali hapo na mtoto akiwa na
uzito wa kilo 3.3.
Dkt. Mbete amesema kuwa lengo la
hospitali yake ni kusaidiana na serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii kuimarisha huduma ya afya ya mama mjamzito na mtoto chini ya miaka mitano
nchini.
Akiongelea gharama, Daktari mfawidhi
amesema kuwa watu wengi wamekuwa wakihofia gharama katika hospitali yake jambo
ambalo si kweli. Amesema kuwa gharama ni ndogo sana akitolea mfano wa gharama
kwa mama mjamzito na watoto chini ya miaka mitano kuwa huduma ni bure. Amesema
kuwa katika hospitali hiyo huduma hiyo hutolewa kwa masaa 24 na kutoa wito kwa
wananchi kujitokeza na kunufaika na huduma hiyo.
Mradi wa Tuunganishe mikono pamoja
ni mradi wa miaka mitatu ukiendeshwa katika mikoa ya iringa, Dodoma, Mwanza,
Mbeya na Morogoro na mashika yanayotekeleza mradi huo Mfuko wa Aga Khan, Wizara
ya Afya na Ustawi wa Jamii, shirika la misaada ya maendeleo la Canada na chuo
kikuu cha Aga Khan.
No comments:
Post a Comment