Mkuu wa Mkoa wa
Iringa, Dkt. Christine Ishengoma amewataka wananchi wa Kata ya Makungu na
Kiyowela kulitumia vizuri bonde la Mgololo kwa kujihakikishia chakula cha
kutosha na kulima klibiashara.
Ushauri huo
ameutoa alipofanya ziara ya siku mbili ya kutembelea, kuhamasisha na kukagua
shughuli za maendeleo katika wilaya ya Mufindi.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma
Dkt. Christine
amesema kuwa ili bonde hilo
liweze kuwa na manufaa kwa wananchi ni lazima litumiwe vizuri kwa wananchi
kulima kwa kufuata nanuni la kilimo bora ili waweze kujihakikishia chakula cha
kutosha. Amesema kuwa uhakika wa chakula cha kutosha ni muhimu sana kumuwezesha mwananchi kutekeleza
majukumu yake ya kujiletea maendeleo. Amesema “ili mtu uweze kufanya shughuli
za maendeleo ni lazima awe ameshiba, ili awe ameshiba, ni lazima awe na chakula
na uhakika wa chakula cha kutosha, hivyo litumieni bonde hili kwa
kujihakikishia chakula cha kutosha”.
Aidha,
amesisitiza kutanuliwa kwa skimu ya umwagiliaji maji katika bonde hilo ili kuongeza
uzalishaji wa mazao. Amesema
“katika kilimo cha umwagiliaji hakuna kupumzika, yaani unapanda, unavuna na
kupanda tena”. Amesema kupitia kilimo cha umwagiliaji, wakulima hao waangalie
kuboresha zaidi kilimo chao na kuwa kilimo cha kibiashara. Amesema kuwa kufanya
hivyo kutawakikishia uhakika wa chakula na kuuza mazao yao jambo
litakalowawezesha kuwa na fedha nyingi kwa ajili ya matumizi mengine.
Akiwasilisha taarifa ya mradi wa
umwagiliaji maji Mgololo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Emelitha Nganung’a amesema
kuwa ujenzi wa banio na mfereji mkuu wa mita 400 ulifanyika mwaka2007/2008
sambamba na barabara ya Lugolofu hadi mashambani yenye km 9 ilitengenezwa.
Mwaka 2009-2011 ujenzi wa mfereji mkuu wenye urefu wa km 4.8 na mifereji ya
kati km 12.33 pia ilijengwa. Amesema kuwa aktika mfereji mkuu madaraja matano
makubwa na madaraja matano madogo yamejengwa. Aidha, amesema vigawa maji 12 na
makaravati 13 vilijengwa. Mifereji ya kati vijawa maji 54 vilijengwa. Mifereji
midogo ilipimwa na kuwa na urefu wa km 23.80. Amesema jumla ya hekta 259
zimepimwa kati ya hekta 600 na wakulima 91 wamegawiwa mashamba.
Akizungumzia ushirika wa wakulima,
Nganung’a amesema kuwa mwaka 2007 wakulima waliunda ushirika wa vijiji vya
Lugolofu na Makungu ambao ni ushirika wa wamwagilia maji Mgololo. Amesema kuwa
idara ya kilimo wilaya ya Mufindi iliwezesha mafunzo ya uundaji na uendeshaji
wa ushirika huo na kufikisha wanachama 788. katika kuleta ufanisi kwa vitendo,
wanachama 50 waliwezeshwa kutembelea skimu ya umwagiliaji ya Igomelo na Uturo
zilizopo wilaya ya Mbalali mkoani Mbeya.
Akielezea shughuli walizofanya
wanachama, amesema kuwa walishiriki katika katika upandaji majani kuzunguka
inteki, kupanga mawe chiin ya kibanio, kufyeka eneo lote la shamba kabla ya
upimaji mifereji midogo ya ndani na kushiri katika uchimbaji wa mifereji midogo
ndani.
=30=
No comments:
Post a Comment