Kituo
cha Afya cha Aga Khan Iringa kwa kushirikiana na Serikali kimetoa huduma za
afya ya mama mjamzito na mtoto katika wilaya ya Mufindi na kufanikiwa
kuwahudumia wananchi wengi kwa wakati mmoja.
Katika
mahojiano na Mratibu wa Mradi wa Tuunganishe Mikono Pamoja nchini, Narmin
Adatia katika kituo cha afya cha Ihongole amesema “lengo la kuweka kambi katika
kituo cha afya cha Ihongole ni kuhakikisha tunawafikia wananchi wengi zaidi kwa
wakati mmoja na kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma ya afya ya mama
mjamzito na mtoto”. Amesema tumeamua kuweka mguvu zaidi kwa wanawake wajawazito
na watoto chini ya miaka mitano kwa sababu kundi hilo linahitaji huduma bora na
salama zinazopatikana kwa urahisi na ukaribu katika maeneo yao. Amesema kufanya
hivyo kunasaidia kufikia malengo ya Milenia katika kupunguza vifo vya wanawake
wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Akiongelea
ushirikiano baina ya Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na
sekta binafsi, Narmin amesifu ushirikiano huo unaogusa ngazi zote za Serikali.
Ameishukuru Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi
kupitia Ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya kwa kuwachagulia eneo kwa ajili ya
kuweka kambi wilayani hapo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi wilayani Mufindi
katika kituo cha Afya cha Ihongole.
Nae
Diwani wa Kata ya Boma, Raphael Makomba amesema kuwa hilo ni jambo jema
lililolenga kuwahudumia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja. Amepongeza
jitihada za kituo cha afya cha Aga Khan kupitia mradi wake wa Tuunganishe
Mikono Pamoja kwa kushirikiana na Serikali ya Wilaya ya Mufindi kuamua kupeleka
huduma hiyo katika Kata ya Boma. Ametumia fursa hiyo kuomba huduma hiyo iwe
endelevu ili kuendelea kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa wakati mmoja.
Morris
Mwingila, mama mjamzito aliyekwenda katika kambi hiyo
kwa
ajili ya kupata huduma ya afya amesifia huduma hiyo na kusema kuwa watoa huduma
walikuwa wamejipanga kikamilifu kuwahudumia wananchi kwa haraka na ubora. “Nilitarajia
kuwa watu tutakaa muda mrefu katika mistari tukisubiri huduma lakini imekuwa
tofauti, watoa huduma wamekuwa wakitoa huduma kwa haraka sana” alisisitiza
Morris.
Huduma
ya Afya kwa Mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano imetolewa bure na
kituo cha Aga Khan Iringa katika kituo cha afya cha Ihongole kwa kushirikiana
na Wilaya ya Mufindi ikiwa ni muendelezo wa huduma hizo chini ya mradi wa Tuunganishe
Mikono Pamoja. Huduma zilizotolewa ni pamoja na uchunguzi wa saratani ya shingo
ya kizazi, unasihi, uzazi wa mpango, upimaji wa CD4 na magonjwa mengine mengi.
=30=
No comments:
Post a Comment