Friday, April 5, 2013

HUDUMA SHIRIKISHI KUKABILIANA NA KIFUA KIKUU



Serikali imeanzisha huduma shirikishi za kifua kikuu na ukimwi kwa lengo la kupunguza makali ya kifua kikuu na Ukimwi kwa wagonjwa wenye magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja.

Kauli hiyo imetolewa na mgeni rasmi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Joseph Muhumba katika hotuba yake ya maadhimisho ya siku ya kifua kikuu Duniani iliyofanyika kwa ngazi ya mkoa katika kijiji cha Lulanzi Wilayani Kilolo.

Muhumba amesema “hivi sasa Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeanzisha huduma shirikishi za kifua kikuu na ukimwi kwa nia ya kupunguza makali ya kifua kikuu na ukimwi kwa waginjwa wenye magonjwa yote mawili kwa wakati mmoja. Wagonjwa wote wa kifua kikuu wanapata ushauri nasaha na kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi”.

Amesema iwapo mgonjwa wa kifua kikuu atagundulika kuwa ana maambukizi ya virusi vya ukimwi atatibiwa kifua kikuu na pia atapatiwa huduma ya dawa za kupunguza makali ya ukimwi. Amesema mtu anayeishi na virusi vya ukimwi atachunguzwa kuona kama ana kifua kikuu na pale atakapogundulika kuwa ana kifua kikuu atapata tiba ya kifua kikuu mapema sambamba na dawa za kupunguza makali ya VVU ili kuboresha afya yake. Amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Iringa kuwa kifua kikuu kinatibika hata kama mtu ana magonjwa yote mawili.

Akiongelea matibabu ya kifua kikuu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo amesema “matibabu ya kifua kikuu huchukua miezi sita. Katika kipindi chote cha matibabu mgonjwa humeza dawa mseto za kifua kikuu chini ya uangalizi wa mhudumu wa afya au msaidizi wa matibabu nyumbani ili kumsaidia na kumpa moyo mgonjwa”. Amewataka wagonjwa wanaoendelea na matibabu wahakikishe wanamaliza tiba kwa muda uliopangwa. Amesema matibabu ya kifua kikuu hutolewa bila malipo katika hospitali zote za Serikali, mashirika ya dini na watu binafsi.

Katika taarifa ya huduma za kudhibiti kifua kikuu kwa Mkoa wa Iringa iliyowasilishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Robert Salim, amesema kuwa huduma za kifua kikuu na kifua kikuu na ukimwi ni ni miongoni mwa huduma za afya ambazo hutolewa kwa nia ya kuboresha afya ya jamii. Amesema huduma hizo hutolewa kupitia mpango wa kitaifa wa kudhubiti kifua kikuu na ukoma chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii uliaozinduliwa mwaka 1977. Amesema malengo ya mpango huo ni kudhibiti na kuzuia kifua kikuu ili kupunguza idadi ya wanaougua na kufariki kutokana na ugonjwa huo kwa njia ya kuhakikisha kuwa huduma bora zinapatikana kwa urahisi na kuwafikia watu wote na hasa wale walioko kwenye hatari zaidi.

Akielezea malengo ya Serikali, Dkt. Salim amesema kuwa Serikali inalenga kupunguza kiwango cha wanaougua na kufa kutokana na kifua kikuu kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2015. Amesema kuwa katika ulimwengu wagonjwa 3,000,000 hugundulika kila mwaka. Aidha, amesema kuwa nchini Tanzania wagonjwa zaidi ya 60,000, wakati mkoani Iringa wagonjwa wanaogulika kwa mwaka ni 2,000 kwa mwaka na kuchangia asilimia sita ya wagonjwa wote nchini kwa mwaka.

Amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo hugundua wagonjwa 300 ambao ni sawa na wagonjwa 130 kati ya watu 100,000. Amesema kuwa idadi ya wagonjwa hutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine. Amesema Halmashauri ya Wilaya ya Iringa (31%), Mufindi (29%), Manispaa ya Iringa (25%) na Kilolo (15%) katika jumla ya wagonjwa wote mkoani Iringa.

Akiongelea mikakati ya kuboresha huduma za kifua kikuu, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameitaja kuwa ni Halmashauri kuwa na mipango ya kuelimisha na kuhamasisha jamii namna ya kushiriki katika kudhibiti kifua kikuu. Mkakati mwingine ni watoa huduma za afya kuzingatia kanuni za kuhisi, kugundua na kutoa matibabu ya kifua kikuu mapema. Mwingine ni wadau wote kushiriki katika kuchangia na kuhakikisha ugonjwa wa kifua kikuu unadhibitiwa na wananchi kuhimizwa kujenga nyumba bora zenye madirisha makubwa ya kupitisha hewa na mwanga.

Maadhimisho ya siku ya kifua kikuu duniani huadhimishwa tarehe 26 mwezi Machi ya kila mwaka na mwaka huu yameongozwa na kauli mbiu isemayo “jukumu la kudhibiti kifua kikuu ni la kila mmoja wetu”.
=30=

No comments:

Post a Comment