Mwenge wa Uhuru unatarajia kuweka mawe ya msingi, kukagua, kuzindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 33 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 4 mkoani Iringa.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa alipokuwa akitoa taarifa ya mkoa wa Iringa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa kupokea Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha IIgomaa wilayani Mufindi uliotokea mkoani Mbeya leo.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dk. Christine Ishengoma amesema “Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika Halmashauri nne za mkoa wa Iringa ambazo ni Mufindi, Iringa, Kilolo na Manispaa ya Iringa tadi tarehe 14 Oktoba, 2013 ambapo mkoa wa Iringa utahitimisha mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa”.
Dk. Christine amesema “Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani Iringa utaweka mawe ya msingi, utakagua, utazindua na kufungua jumla ya miradi ya maendeleo 33 yote ikiwa na thamani ya shilingi 4,721,017,330”. Amesema kuwa akti ya fedha hizo michango ya wananchi ni shilingi 576,317,400, Serikali kuu shilingi 1,251,479,577, Halmashauri 179,470,900 na wadau wa maendeleo 2,713,749,453.
Akiongelea ujumbe wa Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2013, Mkuu wa Mkoa wa Iringa ameutaja kuwa ni “Watanzania ni Wamoja” chini ya kaulimbiu “tusigawanywe kwa misingi ya tofauti zenu za dini, itikadi, rangi na rasilimali”. Amesema kuwa ujumbe huo ni muhimu sana kwa Taifa la Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo watanzania wanatakiwa kushikamana zaidi na kuwa wamoja kuelekea katika mchakato wa kupata Katiba mpya ambayo itakuwa dira ya kuliongoza Taifa.
Akitoa salamu za kuwaaga wananchi wa mkoa wa Mbeya, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kitaifa Juma Ali Simai amekemea vikali wale wote wenye tabia ya kuubeza na kuusemea vibaya Mwenge wa Uhuru kuwa si wazalendo hata kidogo na hawajui msingi wa Uhuru wa Tanzania. Amesema kuwa chimbuko la Mwnge wa Uhuru na Tanzania ni pale Mwalimu Julius Nyerere alipotoa azimio mwaka 1959 wakati akihutubia Bunge la kikoloni na kusema “sisi (watanganyika) tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo pale ambapo pana chuki, heshima ambapo pamejaa dharau”.
Akiongea kwa ukali, Simai amesema kuwa Mwenge ni alama ya Taifa hivyo wale wote wanaopotosha wananchi juu ya Mwenge na kudhohofisha jitihada za kuwaletea wananchi maendeleo kupitia falsafa ya Mwenge wa Uhuru wachukuliwe hatua. Amewataka watu na viongozi wa aina hiyo kujadili amendeleo na wasiotaka watafute Jamhuri yao.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk. Christine Ishengoma (kulia) akipokea Mwenge wa uhuru kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro.
=30=
No comments:
Post a Comment