Wednesday, November 27, 2013

DUNIA AFARIKI DUNIA



 Mhariri Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora, amefariki dunia.
Mzobora (49) alifariki dunia ghafla jana saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi akitokea kwenye Hospitali ya Aga Khan, pia ya Dar es Salaam.

 
                                   Marehemu Dunia Mzobora
 
 Mussa, mdogo wa marehemu, alisema jana kuwa Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku akiwa nyumbani kwake, Tabata Mawenzi, na kupelekwa Aga Khan lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili. Alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.

Mzobora ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya msanifu mkuu, akiwa buheri wa afya.

Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo jijini Dar es Salaam.

Mzobora ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989 akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.

Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.

Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.

Mwaka 1995 alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.

Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi daraja la pili na hadi kufariki dunia kwake alikuwa Mhariri Daraja la Pili.
Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.

Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006 Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika Mawasiliano ya Umma na uandishi wa habari.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema paponi. Amina.


No comments:

Post a Comment