Waombolezaji wakiwa nje ya makazi ya
Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela huko Houghton, Johannesburg,
jana.
Picha na AFP.
Na Neville Meena, Mwananchi
Posted Jumatatu,Decemba 9 2013 saa 9:52 AM
Posted Jumatatu,Decemba 9 2013 saa 9:52 AM
Johannesburg.Makazi ya Rais wa Kwanza mzalendo wa Afrika Kusini yaliyopo
katika Mtaa wa Laa namba 12, Houghton ambako ndiko alikokuwa hadi alipokutwa na
mauti, ni kama hapaingiliki kutokana na wingi wa watu, magari na vyombo vya
habari kutoka sehemu mbalimbali duniani ambavyo vimeweka kambi katika eneo
hilo, usiku na mchana kufuatilia safari ya mwisho ya kiongozi huyo.
Anga la mtaa huo na sehemu za
jirani, limehanikizwa na sauti nyingi za nyimbo zikiongozwa na Wimbo wa Taifa
wa Afrika Kusini ‘Nkosi Sikeleli Afrika’ (Mungu Ibariki Afrika), ukifuatiwa kwa
zamu na nyimbo za kidini na zile za asili ambazo zinasifu ushujaa wa Mandela.
Katika lango la kuingia kwenye
makazi hayo ya Mandela, kuna maombolezo ya aina yake kwani yameambatana na kitu
ambacho kwa macho kinaonekana kama shamrashamra kwa nyimbo za sifa na kufurahia
kile Waafrika Kusini wanachokiita kazi nzuri ya kutukuka ya Mandela aliyoifanya
katika umri wa miaka 95 ya uhai wake.
Mwandishi wetui alitembelea makazi
hayo ya Mandela jana na kushuhudia umati mkubwa wa watu wakifika nje ya nyumba
yake kwa ajili ya kuomboleza; wakiweka mashada ya maua, mishumaa na kadi zenye
ujumbe wa pole kwa familia yake.
Miongoni mwa waliokuwapo katika eneo
hilo ni Mtanzania, Christer Mwageni na watoto wake; Sabina na Faraja.
Mwageni alisema: “Kwa jinsi hali
ilivyo, huwezi kukwepa kuwa mwombolezaji, mimi na wanangu tulikuja hapa
kutembea tu kwa siku tatu hivi lakini tumejikuta tukishiriki msiba na hata kama
tungekuwa hatutaki kushiriki, uhalisia unatulazimisha”.
“Kweli tuna mengi ya kujifunza,
inaonekana msiba huu wa Mzee Mandela umewaunganisha zaidi Waafrika Kusini,
maana wote bila kujali rangi wala kingine chochote, wanaonekana kuomboleza kwa
dhati kutoka mioyoni kabisa.”
Katika eneo hilo la Houghton, ulinzi
umeimarishwa na polisi wako kila kona na wamekuwa wakiwaelekeza waombolezaji na
watu wengine njia sahihi za kufuata hadi kuyafikia makazi ya Mzee Mandela
kutoka na barabara nyingi za kuingia katika eneo kufungwa na nyingine kugeuzwa
maegesho ya magari ya waombolezaji.
Kwa ujumla, pilikapilika ni nyingi,
lakini katika lango kuu la kuingia makazi ya Mandela, ulinzi ni mkubwa na
hakuna anayeruhusiwa kulikaribia isipokuwa wanafamilia, vingozi wa Serikali na
watu wengine wenye shughuli maalumu.
Soweto, Mandela Square
Hali kama hiyo ipo katika makazi
yake ya zamani Mtaa wa Vilakazi Na: 8115, Orlando Magharibi, Soweto ambako kuna
pilikapilika nyingi zinazoyahusisha makundi ya watu kutoka ndani na nje ya
Afrika Kusini.
Mandela aliishi katika Mtaa wa Vilakazi kabla ya kukamatwa na kuwekwa kizuizini na alirejea katika nyumba hiyo miaka 27 baadaye alipoachiwa huru na kuishi humo kwa siku kumi na moja kabla ya kuhamia katika nyumba ya aliyekuwa mkewe, Winnie Mandela katika eneo hilohilo la Soweto.
Kama ilivyo Houngton, katika eneo hilo pia ulinzi umeimarishwa na baadhi ya njia zimefungwa kutokana na wingi wa watu na magari. Vyombo vya habari kutoka kila pembe ya dunia navyo vipo vikiendelea kufuatilia maombolezo hayo.
Katika nyumba ya Soweto ambayo sasa ni makumbusho ya Mzee Mandela, idadi kubwa ya watu wanafurika kujifunza historia ya kiongozi huyo na nje vipo vikundi vinavyoimba nyimbo za maombolezo na kumsifu Mandela kwa ushujaa wake.
Eneo la tatu ni Mandela Square lililopo katika Jiji la Sandton, Johannesburg ambako kuna sanamu kubwa ya kiongozi huyo yenye urefu wa mita sita kwenda juu, likimwonyesha katika hali ya kucheza muziki. Iliwekwa katika eneo hilo, Machi 31, 2004.
Katika eneo hilo, pia ulinzi umeimarishwa na askari wanalazimika kusimamia jinsi watu wanaovyoingia na kutoka. Watu wamekuwa wakisimama katika msitari mrefu kupata fursa ya kupiga picha katika sanamu hiyo yenye uzito wa tani mbili na nusu (kilo 2,500).
Pembezoni mwa sanamu hiyo, kama ilivyo Houghton na Malakazi, limetengwa eneo maalumu kwa ajili ya watu wanaoomboleza kuweka maua, nembo, nyaraka na mishumaa.
Maombolezo ya kifo cha Mandela yanaingia katika siku ya nne leo na yataendelea hadi Jumapili ijayo ya Desemba 15 wakati kiongozi huyo atakapozikwa kijijini kwake Qunu, Mthatha Mkoa wa Eastern Cape.
@Mwananchi
No comments:
Post a Comment