Serikali imepiga
marufuku tabia ya wananchi kukata na kuchoma moto misitu mkoani Iringa ili
kulinda misitu na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.
Marufuku hiyo
imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dkt. Christine Ishengoma katika hotuba
yake ya uzinduzi wa siku ya upandaji miti katika kijiji cha Mtili, wilaya ya
Mufindi.
Dkt. Christine
amesema kuwa juhudi za upandaji miti katika wilaya ya Mufindi ili ziwe endelevu
ni lazima kukomesha tabia ya kukata na kuchoma miti. “Ndugu wananchi, ili
juhudi hizi ziweze kuwa endelevu, natoa wito kwenu kuwa kuanzia sasa iwe ni
mwiko, na aibu kuharibu miti na misitu, kwa kuichoma moto ovyo, kwa kuikata au
kuifyeka ovyo, kuiharibu kwa kuishi ndani ya misitu. Kwa kufanya hivyo utakuwa
umetenda kosa la jinai na unastahili kupewa adhabu kali kwa mujibu wa sheria za
misitu” aliongea kwa ukali Mkuu wa Mkoa. Amesema kuwa iwe tabia na utamaduni wa
wananchi wa wilaya ya Mufindi na mkoa wa Iringa kwa ujumla kutunza miti
iliyopandwa ili kuepuka janga la kuongezeka kwa mabadiliko ya tabia nchi.
Aidha, amewataka wananchi wote kuwa walinzi kwa kuwakamata na kuwaripoti wale
wote watakao kiuka taratibu zilizopo za utunzaji wa misitu kwa mujibu wa
sheria.
Katika risala ya
wilaya ya Mufindi kuhusu siku ya upandaji miti kiwilaya iliyowasilishwa na
Afisa Ardhi na Maliasili wilaya ya Mufindi, Jeswald Ubisimbali amesema kuwa
Halmashauri ya wilaya ya Mufindi imekuwa ikiwashirkisha wananchi wake katika
ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali zilizopo kwa lengo la kutekeleza
mkakati wa taifa wa kupunguza umasikini miongoni mwa jamii (MKUKUTA). Aidha,
ameeleza kuwa lengo kuu la Halmashauri ni kupanda miti zaidi, kuhifadhi
mazngira na maliasili zote zilizopo na kuziendeleza kwa manufaa ya vizazi vya
sasa na vizazi vijavyo.
Akiongelea
ukuzaji wa pato la Halmashauri, Ubisimbali amesema kuwa Halmashauri imejitita
zaidi katika ununuzi wa Ardhi kwa madhumuni ya kupanda miti zaidi ili kukuza
pato la Halmashauri na kuhifadhi mazingira kwa ujumla. Katika kuonesha umakini
wa suala hilo, amesema kuwa Halmashauri imenunua ekari 1,607 katika kijiji cha
Ukani na kufiksha jumla ya ekari 2,771 zinazomilikiwa na Halmashauri ya wilaya
ya Mufindi kwa lengo la kupanda miti.
Aidha, katika
siku ya uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika wilaya ya Mufindi, zaid ya
miti 1,300 ilipangwa chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Iringa.
Katika msimu wa
mwaka 2012/2013 ilipandwa miti 33,445,960 ya aina mbalimbali sawa na hekta
20,903 katika wilaya ya Mufindi.
Ikumbukwe kuwa
wilaya ya Mufindi ina eneo la Misitu la Hekta 203,791 ikiwa ni misitu ya
hifadhi Hekta 57,031, misitu ya Miombo Hekta 80,012 na Hekta 66,748 misitu ya
kupandwa.
=30=
No comments:
Post a Comment