Magdalena Nkulu, Shinyanga
Serikali mkoani Shinyanga imelaani na kukemea tabia
ya baadhi ya wananchi kuvamia maeneo ya migodi kwa lengo la kuiba mchanga wa madini
kwa kuwa ni kinyume cha sheria na hatari kwa maisha ya wananchi hao.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally N. Rufunga akishuhudia shimo hilo
alipotembelea kuona shughuli za wachimbaji haramu katika mgodi wa
Mwadui wilaya ya Kishapu jana, kushoto kwake ni Afisa Tarafa ya Mondo
Bi.Maria Makoye na aliyesimama mbele ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson
Nkhambaku.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Ally Nasoro Rufunga
ametoa tamko hilo alipotembelea Mgodi wa Almasi Mwadui katika wilaya ya Kishapu
jana na kujionea hali ya uchimbaji haramu unavyofanyika katika mgodi huo na pia
kuzungumza na wachimbaji hao wanaojulikana kwa jina la Wabeshi, ambapo amewaahidi
serikali itawasaidia kutafuta shughuli mbadala na kuwataka waachane na shughuli
hiyo mara moja.
Mhe. Rufunga amewaambia wabeshi hao kuwa, serikali
itahahakisha wanapata ajira halali kupitia viwanda vilivyopo na vinavyoendelea kujengwa
mkoani hapa, kuwakopesha mitaji kwa mfuko wa maendeleo ya vijana wa asilimia 5,
pamoja na kufanya taratibu za kuwapatia maeneo madogo ili wachimbe kihalali iwapo
wataacha na biashara hiyo.
Amewaambia kuwa, uchimbaji huo ni kuwaibia wawekezaji
na kuwakwamisha kulipa mapato kwa serikali, kwani nchi inapata kodi kutoka kwa wawekezaji
waliopata leseni halali ya uchimbaji, kodi ambayo inawanufaisha wananchi wenyewe
katika shughuli za maendeleo.
Amewaasa kuacha kutumiwa na watu wenye uwezo kuhatarisha
maisha yao kwa kigezo cha ugumu wa maisha na kusema serikali ya mkoa inawabaini
watu hao na itawashughulikia muda mfupi.
Kwa upande wao wachimbaji hao wamekiri mbele ya
Mkuu wa Mkoa kuwa, ni kweli wanafahamu kazi hiyo si halali na wamemuahidi kuachana
nayo kama watasaidiwa shughuli mbadala kwani wanafanya hivyo kujitafutia riziki
kutoka na hali ngumu ya maisha na masharti ya mikopo kuwa ni magumu.
Kufuatia hali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga amewaagiza
wenyeviti wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui kwanza kutoa elimu kwa wananchi
hasa vijana na kuwakataza kufanya uchimbaji haramu, kwani tabia hiyo imeshaota mizizi
na kuonekana ni halali katika jamii hiyo, pamoja na kuwasidia vijana hao katika
kuibua miradi kutokana na fedha zinazotolewa na mgodiwa Mwadui kila Mwezi. Vilevile,
kuwa na uhusiano mzuri na mwekezaji kwa manufaa ya vijiji hivyo.
Aidha, amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Kishapu
Elisha Nkhamba kusimamia uundwaji wa vikundi vya vijana ili wawezeshwe kufanya shughuli
za kuwaiingiziakipato.
Mhe. Rufunga pia ameutaka uongozi wa Mgodi kuimarisha
ulinzi katika eneo lao kwa kushirikia na Kamanda wa Polisi wa Mkoa.
Amewapongeza na kuwataka kuendelea kuimarisha uhusiano kati ya mgodi na jamii ya
Mwadui kwa kuwasaidia katika shughuli mbalimbali za maendeleo na za kuwainua kiuchumi
wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Nae Meneja Mkuu wa Mgodi wa Mwadui Arlen
Loehmer ameishukuru serikali kwa ushirikiano na kusaidiana kujua na kutatua changamoto
mbalimbali, na anaamini katika mahusiano haya mazuri kunaimarisha juhudi za uwekezaji.
Magdalena
Nkulu,
Afisa Habari
Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa
Shinyanga
0766-289802
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally N. Rufunga akizungumza na wenyeviti wa
vijiji vinavyozunguka mgodi wa Mwadui jana alipotembelea mgodini hapo
kuona uchimbaji haramu unaofanywa na wananchi
wa vijiji hivyo.kushoto kwake ni Meneja mgodi Bw. Arlen Loehmer na
kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kishapu Wilson Nkhambaku
No comments:
Post a Comment