Serikali
imeshauriwa kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuongeza idadi ya shule za sekondari
za bweni na vipaji maalum kutokana na idad ya wanafunzi kufaulu na kupanda kila
mwaka ili kuwatendea haki na kulinda vipaji vya watoto.
Ushauri huo
umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Bibi. Evarista Kalalu wakati akichangia
katika kikao cha uchaguzi wa wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza kwa
mkoa wa Iringa kilchofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo mjini Iringa.
Bibi. Kalalu
amesema ufaulu wa wanafunzi unapanda na kuongezeka lakini sekondari za bweni na
vipaji maalum haziongezeki jambo linalosababisha kutokuwatendea haki wanafunzi
wengi waliofaulu vizuri kukosa nafasi katika shule hizo. Ameshauri kuwa uwepo
mkakati wa kitaifa wa kuongeza shule za bweni na vipaji maalum ili kuwapatia
fursa watoto wengi zaidi.
Wakati huohuo,
Mbunge wa Mufindi Kusini, Bw. Menrad Kigola ameshauli viwepo vyuo vikuu vya
vipaji maalum nchini ili kulinda vipaji vya wanafunzi wanaomaliza shule za
sekondari. “Tunazo shule za sekondari za vipaji maalum chakushangaza watoto
wetu wanapomaliza sekondari wanajiunga na vyuo vikuu vya kawaida jambo
linalochangia kupoteza vipaji vya watoto wetu. Umefika wakati wa serikali kuwa
na vyuo vikuu vya vipaji maalum ili kulnda na kuendeleza vipaji vya watoto
wetu” amesisitiza Bw. Kigola.
Akifunga kikao
hicho, Mwenyekiti wa kikao hicho ambae pia ni Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Iringa, Bibi. Wamoja Ayubu amewataka wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha
wanafunzi wote waliochaguliwa wanaripoti na kuanza masomo shule
zitakapofunguliwa. Aidha, amewataka kuhakikisha vikao vya tathmini ya elimu na
kuzipongeza shule zilizofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi
mwaka 2013.
Bibi. Ayubu
amewata kuweka mikakati endelevu ili mwaka 2014 Mkoa wa Iringa ufikie asilimia
70 ambalo ni lengo la Matokeo Makubwa Sasa kwa mwaka huo. Vilevile, amewataka
kuhakikisha Kata ambazo zimechukua wanafunzi wengi zaidi kuliko uwezo wa vyumba
vya madarasa vilivyopo, kuhakikisha madarasa yanajengwa haraka ili kukidhi
idadi ya wanafunzi stahili. Katika kuendeleza ubora wa elimu mkoani, Kaimu
Katibu Tawala Mkoa amewataka wakurugenzi kuhakikisha usimamizi na ufuatiliaji
unakuwa wa karibu zaidi na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara shuleni ili kuondoa
tatizo la wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika.
=30=
No comments:
Post a Comment