Monday, March 17, 2014

SERIKALI KUSIMAMIA UTUNZAJI VYANZO VYA MAJI



Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa 17/3/2014
SERIKALI mkoani Iringa imejizatiti kusimamia utunzani wa vyanzo vya maji na misitu kwa kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaokiuka na kuharibu vyanzo vya maji.
 
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, Wamoja Ayubu alipokuwa akizindua maadhimisho ya wiki ya maji katika mkoa wa iringa katika kijiji cha Ihimbo wilayani Kilolo.

Wamoja amesema “serikali itachukua hatua stahiki kwa mtu au kikundi cha watu pale itakapobainika kwamba sheria ya utunzaji wa mazingira imekiukwa. Sheria ya mazingira ya mwaka 2002 inakataza shughuli yoyote ya kibinadamu umbali wa mita 60 kutoka ukingo wa mto”. Amewataka wananchi kuzingatia sheria hiyo muhimu ili kuweza kuepuka usumbufu wa kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwezesha utunzaji wa rasilimali maji. 

Akiongelea kaulimbiu ya maadhimisho ya wiki ya maji isemayo uhakika wa upatikanaji wa maji na nishati, amesema kuwa serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kaulimbiu inatekelezwa kwa kulinda sheria mbalimbali za utunzaji wa vyanzo vya maji na misitu. Amesema kuwa kaulimbiu inakumbusha changamoto inayoukabili mkoa ikiwepo ya utunzaji wa vyanzo vya maji kama chemchem, mabwawa, mito na misitu.

Amesema kuwa utunzaji wa rasilimali hizo utauhakikishia mkoa upatikanaji wa maji na nishati. Amesema kuwa maji na nishati vinategemeana na maji yanatumika kama vyanzo vya kuzalisha nishati kama mojawapo ya nishati. Ameongeza kuwa maji hustawisha misitu inayozalisha nishati. Kwa msisitizo amesema kuwa uhakika wa maji na nishati unategemea sana utunzaji wa mazingira.
Katibu Tawala Mkoa wa Iringa amewataka wananchi kudumisha jumuiya za watumia maji kama chombo cha kutunza miradi ya maji. 

Amesema “napenda kuwakumbusha kuwa serikali imejitoa katika kutunza na kuendesha miradi ya maji” amesisitiza Wamoja. Amesema kuwa ni jukumu la jamii nzima kuunga mkono jumuiya za maji zinazoundwa katika maeneo yao. Amewataka kutimiza wajibu kwa kutoa michango inayohitajika na waliyojipangia katika jumuiya zao.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya upatikanaji huduma ya maji katika mkoa wa Iringa kwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji mkoani Iringa, Mhandishi wa Maji mkoa wa Iringa, Shaban Kitambulio Jellan amesema kuwa wananchi wanaopata huduma ya maji safi mijini katika mkoa wa Iringa ni 189,644 kati ya wananchi 247,156 ambayo ni sawa na asilimia 76.7 ya wananchi wote waishio mijini.

Aidha, hali ya huduma ya maji inategemewa kuongezeka mara baada ya kutekelezwa kwa miradi katika miji ya Ilula, Kilolo na Mafinga. Amesema kuwa miradi hiyo inategemewa kutekelezwa kupitia progrmu ya maendeleo ya sekta ya maji (WSDP) na wananchi wapatao 57,512 wanatarajiwa kupata huduma bora ya maji safi na salama.

Akiongelea ujenzi wa miradi ya matokeo makubwa sasa (BRN), Mhandishi Jellan amesema kuwa mkoa unajenga miradi 42 ya maji yenye kuleta matokeo makubwa sasa. Amesema kuwa miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za ujenzi. Amesema kuwa mkoa wa Iringa unahitaji kiasi cha Tshs. Bilioni 11.582 kwa ajili ya kuwalipa makandarasi, wataalamu waelekezi na usimamizi na ufuatiliaji wa ujenzi wa miradi hiyo.
=30=

No comments:

Post a Comment