Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Viongozi wa dini mkoani Iringa
wametakiwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali kuhakikisha maisha bora
kwa wananchi yanawezekana.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa
wa Iringa, Bibi. Amina Masenza alipokuwa akiongea na viongozi wa dini katika
kikao maalumu kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Bibi. Masenza amesema kuwa viongozi
wa dini ni muhimu sana katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na serikali na
kufikisha ujumbe kwa watu wengi. Amesema “viongozi wa dini mnao watu wengi
nyuma yenu ambao ni waumini na wanawasikiliza hivyo mnawajibu wa kusaidia
juhudi zinazofanywa na serikali za kuboresha maisha ya wananchi wake”.
Akiongelea zoezi linaloendelea la
uboreshaji daftari la wapiga kura, Mkuu wa Mkoa wa Iringa amesema kuwa zoezi la
uboreshaji daftari la wapiga kura linaendelea katika mkoa wa Iringa. Amesema
kuwa changamoto ni kuwa mashine zinatumia umeme hivyo zinahitaji kuchajiwa na
sehemu za vijijini hazina umeme. Amesema kuwa mkoa unakabiliana na changamoto
hiyo ili kuhakikisha zoezi zima linakuwa na mafanikio. Amesema changamoto ya
matumizi ya kopyuta limechukuliwa kwa uzito unaostahili na watu wenye uelewa wa
kompyuta wamechukuliwa katika kufanya zoezi la uboreshaji daftari hilo ili liende
vizuri na haraka.
Wakati huohuo, bibi. Masenza
amewataka viongozi wa dini kuendelea kuwahamasisha waumini na wananchi kwa
ujumla kuipitia na kuifahamu Katiba inayopendekezwa ili mwisho waweze kufanya
maamuzi sahihi wananchi wenyewe pasipo kushurutishwa. Amesema kuwa Katiba hiyo
imegusa maeneo na makundi yote ya kijamii hivyo ikisomwa kwa umakini
itawasaidia wananchi ufanya maamuzi sahihi.
Katika kikao hicho mada juu ya hali
ya lishe katika mkoa, hali ya maambukizi ya ukimwi na hali ya elimu
ziliwasilishwa na kujadiliwa kwa kina. Viongozi hao wamekubaliana kukutana kila
baada ya miezi nne na kujadili mambo muhimu katika mkoa wa Iringa.
=30=
No comments:
Post a Comment