Thursday, May 28, 2015

IRINGA WATAKIWA KUJIANDIKISHA DAFTARI LA WAPIGA KURA




Na. Ofisi ya Mkuu wa Mkoa
Wananchi wa Mkoa wa Iringa wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika wiki ya mwisho ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.

Kauli hiyo imetolewa na Mratibu wa Mkoa wa zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura, Bw. Wilfred Myuyu katika mahojiano maalumu ya hali halisi ya zoezi hilo katika mkoa wa Iringa yakiyofanyika ofisini kwake leo.
 
Mratibu wa zoezi la uboreshaji daftari la wapiga kura mkoa wa Iringa, Bw. Wilfred Myuyu
Bw. Myuyu amesema kuwa lengo la Tume ya Taifa ya uchaguzi ni kuhakikisha kila mtanzania mwenye sifa anaandikishwa katika Daftari hilo la kudumu. Amesema kuwa Mkoa wa Iringa pia umedhamilia kuandikisha wananchi wote wenye sifa katika daftari hilo. Ametoa wito kwa wananchi wote wenye sifa kujitokeza mapema katika zoezi hilo ili waweze kuandikishwa. Amewataka wananchi kujiandikisha mapema na kuacha tabia ya kusubiri siku ya mwisho ambapo watu huwa wengi katika mistari ya uandikishaji. 

Akiongelea hamasa ya wananchi katika mkoa wa Iringa, Mratibu wa Mkoa amesema kuwa hamasa ni kubwa kwa wananchi wa Mkoa wa Iringa. Amesema kuwa mkoa umepanga awamu nne za uandikishaji. Amezitaja awamu hizo kuwa ni awamu ya kwanza iliyoanza tarehe 30/4/2015-6/05/2015, awamu ya pili 8/5/2015-14/5/2015, awamu ya tatu 16/5/2015-22/5/2015 na awamu ya nne 24/5/2015-30/5/2015. Amesema kuwa katika awamu tatu zilizopita hamasa ya wananchi imekuwa ni kubwa. “Hadi kufikia tarehe 22/5/2015 jumla ya wapiga kura 391,579 sawa na asilimia 79.3 ya lengo la uandikishaji mkoa walikuwa wamejiandikisha”.
 
Bw. Myuyu amesema kuwa changamoto kubwa ni wingi wa watu wanaopenda kujiandikisha siku ya mwisho na vituo kulazimika kuongeza muda wa uandikishaji. Amesema kuwa awamu ya mwisho itatoa matokeo mazuri.
Bw. Myuyu ametoa wito kwa wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu katika zoezi hilo ili liwe la mafanikio na kuwataka kuwaibua wale wote wasio na sifa za kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura.

Awali Bibi. Rehema Mohamed Sadiki, mkazi wa mtaa wa Maliwa amepongeza zoezi la uandikishaji katika mtaa wake na kusema kuwa waandikishaji wapo makini na wana kasi ya kulidhisha. Aidha, ametoa rai kwa wananchi wote kujitokeza mapema kuboresha taarifa zao kabla ya siku ya mwisho ili kuweza kutumia fursa na haki yao kikatiba ya kuchagua viongozi wanaofaa.

Zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura limeanza tarehe 30/4/2015 Mkoani Iringa na linatarajiwa kumalizika tarehe 30/5/2015 wakati mkoa ukitarajia kuandikisha wapiga kura 493,277.
=30=

No comments:

Post a Comment